DIRISHA la usajili bado halijafunguliwa lakini tayari timu mbalimbali zimeanza kufanya usajili huku Simba kukiwa na maombi ya wachezaji 11 wanaotaka kujiunga na timu hiyo.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Zacharia Hanspope huku akitamba hawana haraka ya kusajili pamoja na kupokea maombi hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hanspope alisema hata ukiwa na pesa nyingi lakini huna maarifa ya kutengeneza timu bora ya ushindani ni sawa na bure huku dongo hilo akilitupa kwa watani zao Yanga baada ya siku chake kuingia mkataba wa Sh 41 bilioni na Azam Media.
Alisema endapo klabu za Ligi Kuu Bara zitashindwa kujizatiti na kufanya usajili kwa kufuata mahitaji ya benchi la ufundi wataendelea kutwaa mataji kila msimu na wao watabaki kuwa wasindikizaji.
Alisema uwekezaji ndani ya klabu yoyote ni kwa ajili ya kuimarisha timu, lengo ni kuonyesha ushindani na kukuza klabu iweze kuingia kwenye ushindani kimataifa na ligi ya ndani huku akifafanua wao sasa wanataka kuwa klabu bora Afrika na ligi ya ndani tayari wamejipima na kuona wamepiga hatua zaidi.
“Hadi sasa nina majina ya nyota 11 wa kimataifa wanaomba nafasi ya kuitumikia Simba msimu ujao hivyo, wanaosema timu yetu imeshindwa kufikia dau na kuachana na mchezaji si za kweli, tunaweza kumsajili yeyote atakayehitajika na benchi la ufundi kwa gharama yoyote.
“Sijaona mwendelezo mzuri wa usajili bora kwenye timu kama ilivyokuwa Simba ndani ya misimu minne sasa tuliyofanikiwa kutwaa taji na endapo klabu zitashindwa kujizatiti basi Simba itaendelea kutawala kwa misimu mingine mingi inayokuja,” alisema
Alisema ubora wao ndani ya miaka hiyo hakuna mchezaji ambaye hana matamanio ya kucheza Simba wakiwemo wa kigeni hivyo hawaoni nafasi ya kukosa mchezaji kutoka mataifa wanayotamani kupata mchezaji huku akiweka wazi kuwa labda wachezaji wa ndani.
Kiongozi huyo alisema kwa levo waliyonayo sasa hawapo tayari kushindana na hawababaishwi na tetesi wanachokifanya ni utekelezaji mambo yakiwa sawa na muda ukifika nyota wapi waliowasajili ndio watakapowaweka wazi kwaajili ya utendaji kazi.