Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Hans Pluijm amesema ameanza kukisuka kikosi chake kuelekea mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC utakaopigwa Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, Agosti 10.
Singida imerejea mazoezini rasmi juma hili ikianza maandalizi kuelekea msimu ujao lakini kocha huyo ameeleza kuwa wanahitaji kufanya vizuri kwanza kwenye mechi za Ngao ya Jamii kabla ya msimu kuanza, hivyo wanajipanga vilivyo.
“Tumeanza maandalizi rasmi wiki hii na tayari wachezaji wetu wengi wa nje ya nchi wameanza kuwasili, tunahitaji kuwa na maandalizi mazuri zaidi kwa sababu tuna mtihani kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC.
“Kila mtu anafahamu Simba SC ni wazuri, wanaendelea kujipanga kuelekea msimu ujao, nasi pia tunaisuka timu kwa ajili ya msimu mpya ambao tutashiriki michuano mingi, ni lazima tuwe na kipimo cha ubora wa sawasawa na kuanza lazima tujipange kufanya vizuri dhidi yao,” amesema Pluijm.
Singida ambayo msimu ujao kwa mara ya kwanza itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Julai 10 itafungua dimba kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga huku Young Africans wakicheza na Azam FC katika uwanja huo huo.