Mshambuliaji wa Ivory Coast, Sebastian Haller amekuwa gumzo katika vyombo vya habari na hii ni baada ya kuisaidia nchi yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).
Mwamba huyu anayekipiga Borussia Dortmund aliisaidia nchi yake kutwaa ndoo hiyo baada ya kupachika bao la pili la ushindi dakika 81, Jumapili, jijini Abidjan. Shujaa huyu ameifanya nchi yake kuweka rekodi kutokana na ukweli mara ya mwisho nchi mwenyeji kutwaa ubingwa ni Misri mwaka 2006.
Gumzo la mshambuliaji huyu linavuma zaidi kwa sababu miezi 18 iliyopita alikuwa katika vita ngumu na kubwa mara baada ya kugundulika kuugua saratani ya kokwa ya kiume.
Ikumbukwe kwa binadamu kupona saratani na kurudi kuendelea na soka sio jambo dogo, hii ni kwa sababu ya kutibiwa na dawa kali ambazo huwa na madhara katika hatua za awali.
Itakumbukwa hata katika mashindano haya hakuweza kucheza katika mechi za hatua ya awali kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu.
Tatizo hili lakifundo nalo lilimsumbua katika miezi ya karibuni kabla ya kuanza kwa Afcon 2023 na mshambuliaji huyu nyota anayemhusudu na kumwiga Didier Drogba, sasa ameithibitishia dunia mchezaji mkali aliyeishinda saratani na amebeba ubingwa.
HISTORIA YA KUUGUA SARATANI
Haller alitua Dortmund Julai mwaka jana kwa Pauni 31 milioni akitokea Ajax. Baada ya wiki mbili akiwa katika mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya Switzerland alilalamika ana maumivu ya chini ya tumbo.
Alionana na daktari wa mfumo wa mkojo aliyebainika ana uvimbe wa saratani katika kokwa ya kiume tatizo linalojulikana kitabibu kama ‘Testicular tumour’.
Alilazimika kulazwa wiki mbili kutokana na matibabu kadhaa ikiwamo kufanyiwa upasuaji na kutumia dawa za saratani. Hii ilisababisha kwenda hospitalini mara kwa mara kupata matibabu na kufuatiliwa maendeleo yake.
Alitumia miezi kadhaa na matibabu ya dawa akiweka pembeni majukumu yote ya soka katika klabu hiyo na baadaye madaktari walimweleza amefanikiwa vita hiyo.
Desemba mwaka jana alielezwa yuko salama kurudi uwanjani na kuendelea kucheza soka bila tatizo lolote.
Hii ilikuwa ni taarifa nzuri sana kwake yeye na familia yake ikiwamo mke wake ambaye hakuamini wakati alipopokea simu ya Haller kumjulisha kuwa amegundulika ana saratani.
Saratani ni moja ya matatizo ambayo huwa kupona kwake ni bahati, unaweza kuwa na mamilioni ya pesa ya kujitibu katika sehemu yoyote duniani lakini saratani ikipiga hatua za mbeleni ni ngumu kupona.
Bahati ilikuwa nzuri kwa Haller kwani saratani yake ilikuwa katika hatua za awali ambayo inatibika kwa matibabu ya dawa na upasuaji.
Kwa wale wafuatiliaji wa muziki mtakumbuka, Rene Angelil ambaye alikuwa mtayarishaji wa muziki na mume wa mwanamziki maarufu Celine Dion alifariki dunia kutokana na saratani.
Mtayarishaji huyu tajiri aliwahi kuweka dau la Dola 2 milioni kwa daktari yeyote duniani atakayeweza kumtibu na kupona tatizo hilo, lakini wapi kwani hakuna daktari aliyeweza kumtibu.
Hapa unapata picha Haller ametoka katika vita ya namna gani. Na ilikuwa bahati kwake kwani tatizo hilo liligundulika katika nchi ambazo zina huduma za hali ya juu za tiba.
Akiwa anapambana na tatizo hilo hakukaa tu kujitibu, pia alikuwa sambamba na mkufunzi wake binafsi wa mazoezi ambaye alikuwa akimpa mazoezi maalumu kuendana na hali aliyokuwa nayo.
Alipomaliza matibabu hayo walikuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia pamoja na mkufunzi huyo. Alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo, mkufunzi huyo alisema yalikuwa ni mazoezi ya kumwondolea uchovu.
Vile vile na madaktari nao walimshauri kuwa asikae na kuwaza jambo hilo, alitakiwa kujichanganya na jamii ili kumwepusha na msongo wa mawazo.
Haller ni mzaliwa wa Ufaransa mwenye asili ya Ivory Coast upande wa baba, alijichanganya mtaani kwao kusini mwa Ufaransa katika Mji wa Cannes na marafiki zake wakicheza golf na michezo ya baiskeli.
Hata katika tuzo za Ballon d’Or zilizofanyika Ufaransa mwaka huo alijichanganya katika sherehe hizo akiwa na wadogo zake wa kuzaliwa. Alifanikiwa kushika nafasi ya 13 katika tuzo hizo yakiwa ni mafanikio alipokuwa na Ajax msimu wa 2021/2022.
Alipewa nafasi ya kwenda mbele katika tuzo hizo akionekana kutokuwa na nywele zote za usoni hiyo ni kutokana na madhara machache ya dawa za matibabu za saratani.
Aliongea kwa kujiamini kama vile hakuwa katika matibabu hayo, aliwaeleza watu waliohudhuria yuko imara na anaendelea vizuri. Alisema amefurahi na ilikuwa muhimu kuwepo hapo.
Daktari aliyekuwa anamtibu, Dr. Groticke na Profesa Laura-Maria Krabbe alieleza walitumia saa nne kuondoa uvimbe huo na huku akipewa mizunguko kadhaa ya tibakemikali ya saratani.
Desemba 20 mwaka jana alipewa taarifa ya kuthibitisha sasa yuko timamu kiafya na anaweza kuendelea na soka. Alikwea mwewe kujiunga na klabu hiyo iliyokuwa Hispania katika maandalizi.
Aliwaambia wenzake kichwani mwake suala la kustaafu soka kwa tatizo hilo halitawezekana. Siku tatu baadaye katika mechi ya kirafiki nchini Uswisi alifunga ‘hat-trick’ mchezo walioshinda 6-0.
SIRI YA UBINGWA HII HAPA!
Tangu mwanzo mwa mashindano haya hadi yanaisha, mtu aliyekuwa na hekaheka nyingi nje na ndani ya uwanja ni aliyekuwa staa wa nchi hiyo, Didier Drogba.
Alikuwa akitumiwa kuleta ari na hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo pamoja na mashabiki. Hata katika fainali hiyo walipokomboa aliwaonyesha ishara mashabiki kuwahimiza kushangilia.
Ndiye nyota wakuigwa wa Hallier aliyemwambia asijali atapona tatizo hilo na atafanya mengi katika soka.
Hata alipoitwa kushiriki Afcon 2023 alimwambia umeishinda saratani sasa ni wakati wa kuisadia nchi kushinda kombe hilo na hilo likatokea.
Kitendo cha kumtumia Drogba kujenga saikolojia ya wanasoka wa Tembo wa Afrika ilikuwa ni moja ya mbinu zilizofanikiwa kusaidia kuleta mshikamano wa timu hiyo.