Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna wa kumcheka mwenzake, wote sasa wanapiga hesabu za vidole

Simba Yanga Cafcl Hakuna wa kumcheka mwenzake, wote sasa wanapiga hesabu za vidole

Mon, 11 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tuanze Kumasi pale Ghana katika mji ambao upo kilomita 247 kutoka Jiji Kuu la Accra. Ijumaa jioni ambayo Nickson Kibabage angeweza kuvunjwa mguu na beki mmoja wa Medeama huku mwamuzi akishuhudia lakini mwamuzi huyo akaishia kutoa kadi ya njano tu.

Na baadaye Kibabage ambaye alikuwa anacheza nafasi hiyo kwa sababu beki mwenzake wa kushoto, Joyce Lomalisa nusura avunjwe mguu na Percy Tau katika Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki moja kabla ya hapo, alijikuta akifunga bao halali ambalo lilikataliwa na mshika kibendera kwa madai ya kuwa alikuwa ameotea.

Matukio mawili ambayo yangeweza kuifanya Yanga iondoke na pointi tatu pale Kumasi katika mkakati wao wa kuchukua pointi sita kutoka kwa Medeama baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly Uwanja wa Taifa wiki iliyopita.

Haikuwezekana ingawa Yanga walimiliki mpira vema hasa katika kipindi cha pili na kuendelea kuonyesha ubabe wao katika viwanja vya ugenini. Mpira wetu umebadilika. Yanga ilipofungwa mabao 3-1 na CR Belouzidad walitawala mpira. Na hata Jumamosi jioni ilitawala mpira.

Na sio wao tu. Turudi mpaka pale Marrakech Morocco jiji lililo kilomita 242 kutoka katika Jiji Kuu la Morocco Casablanca. Simba ilicheza mpira mkubwa ambao sijawahi kuuona ikiucheza kwa kipindi cha miezi 15 iliyopita tangu ilipoanza kusuasua katika soka letu.

Kipa Ayoub Lakred alipangua penalti halali ya kipindi cha kwanza kutoka kwa Waarabu, lakini kiwango chake kwa ujumla kiliendana na timu. Simba hii tulikuwa hatujaiona kwa muda mrefu ingawa Clatous Chama alianzia benchi.

Ilikuwa bora wakati ikiwa na mpira na bado ilikuwa bora wakati ikiwa haina mpira. Wakati ikiwa na mpira haikuupoteza kiurahisi. Ingeweza kupiga hadi pasi saba. Wakati ilipokuwa haina mpira ilirudi kujipanga kwa haraka na kuutaka mpira. Ni kitu ambacho haikuwa nacho katika siku za karibuni hasa siku ile iliyoadhibiwa mabao matano na mtani wake pale Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Utazungumzia kushuka viwango vya timu za Pembe ya Kaskazini mwa Afrika, ni kweli. Wydad hii sio bora sana. Hata Al Ahly ya leo sio bora sana. Lakini haiondoi ukweli kwamba timu zetu kwa sasa zinafurahia kucheza na wakubwa hawa kwa sababu zina wachezaji wenye viwango na wenye kujiamini. Simba ilionyesha hilo kwa mara nyingine juzi usiku pale Marrakech.

Tayari ilishaonyesha katika mechi mbili ambazo ilicheza na Wydad msimu uliopita na nusura itinge nusu fainali. Safari hii ilionyesha tena kwa Wydad ingawa bao la dakika za mwisho ziliwaacha wachezaji wakilia katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Na sasa timu zetu zote mbili zimekaa katika mtego wa panya. Simba ni wa mwisho katika kundi lake ikiwa na pointi mbili baada ya kutoka sare mbili na kufungwa mechi moja. Yanga nayo ina pointi hizo hizo na katika matokeo kama hayo hayo. Nafasi yao katika kundi lake ni hiyo hiyo.

Wote wawili wameanza kutegemea hesabu za vidole kuweza kufuzu katika hatua ya robo fainali. Kundi la Yanga linaongoza kwa kukaa kimitego zaidi. Anayeongoza ana pointi tano. Ameachana pointi tatu tu na Yanga. Wanaofuata wana pointi nne ambao ni Belouzidad na Medeama. Wana pointi nne.

Nini kifanyike? Yanga ishinde mechi inayofuata ya nyumbani dhidi ya Medeama, halafu ipumzike kidogo hadi Februari ashinde tena nyumbani dhidi ya Belouzidad iwe na pointi nane. Kutokana na ugumu wa kundi lake kuna uwezekano pointi nane zikakupitisha katika kundi au zikasababisha hatima iende katika mechi ya mwisho.

Tatizo kubwa la kundi la Yanga halina mbabe. Kushuka kwa viwango vya Waarabu vimeharibu makundi. Fikiria namna ambavyo Wydad imefungwa mechi mbili mfululizo katika kundi lake, halafu Al Ahly ametoa sare mbili mfululizo. Zamani tulikuwa tunampisha mkubwa aende zake kileleni kwa mbali halafu wengine tunawania nafasi ya pili.

Kwa sasa hauwezi hata kujua ambacho kinaweza kutokea pindi Al Ahly ikienda Algeria wiki ijayo. Ingekuwa bora kwa Yanga kama Al Ahly angefanikiwa kumpiga Belouzidad nje na ndani ili amvunje miguu lakini kwa sasa kundi linakuwa gumu kwa sababu lina sare nyingi.

Hauwezi hata kujua pambano la Medeama na Al Ahly pale Kumasi litakuwaje. Ni kama ambavyo hata hauwezi kujua pambano la Yanga na Al Ahly litakuaje pale Cairo. Sio lazima kwa Yanga kupoteza pambano hilo la mwisho lakini kwa sasa kitu cha msingi ni kushinda mechi zake mbili za Dar es Salaam.

Kundi la Simba nalo lina hesabu za vidole. Walau ASEC imejipambanua kuwa ni wababe wa kundi mpaka sasa. Kinachotakiwa ni Simba kushinda mechi zake mbili za nyumbani dhidi ya Wydad kisha Jwaneng Galaxy. Ninachoona ni kwamba nafuu ya Simba inaweza kuwa itasafiri kwenda Abidjan huku tayari ASEC ikiwa imefuzu.

Jumamosi ASEC imeipasua Jwaneng, ugenini na kuna kila dalili itashinda tena katika pambano la marudiano ikiwa nyumbani. Itakuwa na pointi 10 ambazo kwa kiasi kikubwa zitakuwa zimeihakikishia kufuzu. Sidhani kama itabana meno sana akicheza na Simba mechi ya mwisho.

Vyovyote ilivyo kwa sasa mapacha wa Kariakoo wamebakiza matumaini ya kushinda mechi zao mbili za nyumbani. Wasikosee sana katika mechi hizi na kuna matumaini wanaweza kufanya jambo. Inawezekana lakini wanahitaji kuwa waangalifu zaidi na pia kuanza kufanya maombi katika mechi ambazo haziwahusu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live