Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna namna, ni alama tatu tu

Yanga Yanga Kkosi cha Yanga

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa nini Yanga inapaswa kushinda leo dhidi ya Real Bamako kwenye Uwanja wa Mkapa? Kwanza, watafikisha pointi saba ambazo itakuwa imebaki tatu tu wafuzu robo fainali. Pili, itawapa mzuka dhidi ya Monastir mechi ijayo ambayo wakimfunga wanafuzu moja kwa moja. Kwa hiyo kilichobaki ni Dijei kuwaleta uwanjani saa 1 usiku tushudie kandanda.

Timu hiyo ya Mali iliyochomoa dakika za mwisho kwenye mechi ya awali na kulazimisha sare ya bao 1-1 kwao, wamesisitiza kwamba mchezo wa leo wataucheza kama fainali ingawa Yanga wamepania kuonyesha ubora wao.

Yanga ambayo inashika nafasi ya pili katika Kundi lao D hakuna kitu cha maana watakihitaji zaidi ya ushindi pekee kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 4 kabla ya mchezo wa leo.

Endapo Yanga watashinda mchezo wa leo watafikisha pointi 7 ambazo ni kama zitawaondoa TP Mazembe ambao baadaye leo usiku watakuwa ugenini dhidi ya US Monastir ambao ndio vinara wa kundi lao huku Bamako wakishika mkia wakiwa na pointi 2 ambazo walizipata kwenye mechi mbili za nyumbani alizopata sare zote.

Baada ya kuwachapa kibabe nyumbani TP Mazembe kwa mabao 3-1 Yanga itakuja na hasira ya kusahihisha makosa yake baada ya kupata sare ambayo waliamini wangeshinda mechi dhidi ya Bamako.

Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi baada ya kuwapumzisha kiakili wachezaji wake ameliambia Mwanaspoti kuwa wanakwenda kucheza fainali katika mchezo ambao utaamua uwezekano wao wa kutinga hatua inayofuata.

Nabi alisema; "Jambo zuri kwetu ni kwamba wachezaji walipata muda mzuri wa kupumzika na wameimarika wale ambao walikuwa na maumivu nao wameimarika, hii ni fainali ya hatma yetu katika safari tunayotaka kwenda, tunajisahihisha ni wakati wao wachezaji wetu kuonyesha ukubwa wao."

"Tunakwenda kucheza na timu isiyotabirika, sote tunajua ni mazingira gani tunatakiwa kuwa nao makini lakini pia wachezaji tumewapa mbinu za kutumia makosa yao, tunatakiwa kuamua mchezo kwa kushinda mapema lakini pia tunatakiwa kuhakikisha hatujiweki katika mazingira magumu kwa makosa yetu,"alisema Kocha huyo.

Kocha wa Bamako, Nouhoum Diane alisema baada ya kushindwa kushinda katika mechi zao tatu zilizopita watakuwa na dakika 90 pekee za kuamua hatma yao dhidi ya Yanga na kwamba hawatakuja na akili ya kujilinda.

"Tulishashindwa kushinda kwenye mechi tatu, hii ni mechi ya kuamua kurudisha matumaini yetu au vinginevyo, haitakuwa rahisi lakini hatutakuwa na cha kupoteza wala kuamua kujilinda tena tutapambana uwanjani,"alisema Diane ambaye ni kocha mzawa anayeheshimika nchini humo.

Mualgeria kati

Mchezo huo ambao utaanza majira ya saa 1:00 usiku utaamuliwa na mwamuzi kutoka nchini Algeria, Mustapha Ghorbal akiwa mwamuzi wa kati huku akisaidiwa na Mokrane Gourari na Abbes Zerhouni huku mwamuzi wa nne akiwa Loutfi Bekouassa ambao wote wanatoka Algeria

Refa Ghorbal amekuwa na historia ya kumwaga kadi na hivyo Yanga wanapaswa kuwa makini. Kuthibitisha jinsi refa huyo alivyo mwepesi wa kutoa kadi, katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika, ametoa jumla ya kadi 56 ambazo ni sawa na wastani wa kadi 5.6 kwa mechi, kati ya hizo, kadi za njano ni 53 na kadi nyekundu ni tatu.

Makocha wakubwa jukwaani

Utamu mwingine ni uwepo wa makocha wakubwa watakoushuhudia mchezo huo ambapo kocha wa zamani wa Chelsea ambaye anaifundisha timu ya taifa ya Zambia Avram Grants atakuwa jukwaa kuu akimsoma mshambuliaji wake Kennedy Musonda ambapo mapema Musonda ametuma salamu akisema "Tuko tayari wananchi njooni muwe mashahidi kesho (leo)".

Mbali na Grants pia kocha mpya wa Taifa Stars Adel Amrouche ambaye baada ya kutambulishwa jana jijini Dodoma kisha kusafiri kuiwahi Simba jana ikicheza dhidi ya Vipers, leo pia ataishuhudia Yanga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live