Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna namna! Mastaa hawa ilikuwa lazima wasepe

VIDEO: Tazama Luis Miquissone Alivyoanza Mazoezi Na Simba Luis Miquissone

Thu, 27 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kuna muda mpira wa miguu huwa na matukio ya kikatili sana kwa wale wanaoufuatilia. Achana na habari za matokeo, matukio haya ya kikatili muda mwingine hutokea hata kwenye usajili na mambo mengine ya nje ya Uwanja.

Hivi karibuni stori kubwa imekuwa ni tetesi za kuondoka kwa straika wa Yanga Fiston Mayele anayehusishwa na Pyramid.

Hakuna shabiki wa Yanga anayetamani kuona fundi huyu akiondoka lakini ndio hivyo lazima mpira uonyeshe ukatili wake.

Ikiwa staa huyu ataondoka hii haitokuwa mara ya kwanza mashabiki wa Simba na Yanga kushuhudia mchezaji tegemeo na wanayempenda akiondoka kwa sababu timu zao zimeshindwa kuwauzia kutokana na nguvu kubwa kiuchumi ya timu zilizowahitaji.

Iliwahi kutokea mara kadhaa huko nyuma na huu ni muendelezo wake tu, leo tunakuletea baadhi ya mastaa wengine ambao ilishindikana kubakishwa na wakasepa zao wakati bado mashabiki wakiwahitaji.

CHAMA - SIMBA

Agosti 11, 2021 ilikuwa ni siku ya machungu makali kwa mashabiki wa Simba baada ya kuuzwa rasmi kwa kiungo pendwa Clatous Chama aliyenunuliwa na RS Berkane ya Morocco.

Ilikuwa ni taarifa ya kuumiza kwa mashabiki wa timu hiyo lakini kulikuwa hakuna namna kwani Berkane iliweka mkwanja wa maana mezani na Simba kushindwa kumbakisha kwa namna yeyote ile.

Wakati Chama anaondoka Simba alikuwa amefanya makubwa mengi kwenye msimu uliokuwa umemalizika kwa kuibuka kinara wa asisti kwenye ligi akifanya hivyo mara 15 na kupachika mabao manne.

Haikuishia hapo Chama aliwakonga nyoyo mashabiki wa Simba kwenye Ligi ya Mangwa Afrika akiisaidia Simba kufika robo fainali kwa msimu ule huku yeye akifunga mabao matano na kutoa asisti tatu. Kwa sasa Chama yupo Simba baada ya kushindwa maisha ya Morocco na kurejea Unyamani.

Wakati huo chama aliuzwa Berkane kwa Dola 600,000 sawa na takribani Sh1.3 bilioni kama ada ya uhamisho kwa kipindi hicho, fedha ambazo ni ngumu kuziacha.

MAKAMBO - YANGA

Mashabiki wa Yanga Agosti 10, 2019 ilikuwa ni zamu yao kulia baada ya kuuzwa rasmi kwa aliyekuwa mshambuliaji wake Mkongomani Heritier Makambo kwa Horoya ya Guinea.

Wakati huo Yanga ipo kwenye 'Njaa', Makambo ndiye alikuwa staa wa timu hiyo akifunga na kushangilia kwa staili yake ya 'Kuwajaza' lakini mwisho wa siku akauzwa kutokana na Yanga kushindwa kumbakisha kikosini hapo.

Kabla ya kuuzwa, Makambo alikuwa ameifungia Yanga mabao 19 na kuwa mfungaji bora wa timu hiyo kwa msimu wa 2018/2019.

Makambo aliuzwa Horoya kwa dau la Dola 100,000, sawa na sh 245 milioni.

MIQUISSONE - SIMBA

Agosti 2021 ulikuwa ni mwezi wa maumivu makali kwa mashabiki wa Simba, baada ya Agosti 11, kuumia kwa kuuzwa kwa Chama, Agusti 26 walilizwa tena baada ya winga wake hatari kutoka Msumbiji, Luis Miquissone kuuzwa rasmi Al Ahly ya Misri.

Baadhi ya mashabiki waliwatupia lawama viongozi wa Simba kuruhusu kuondoka Chama na Luis kwa wakati mmoja licha ya kwamba viongozi hao hawakuwa na la kufanya kutokana na kushindwa ubavu wa kifedha na Waarabu.

Kabla ya kuondoka Simba, Miquissone alikuwa amewasha moto sana katika msimu wake mmoja ndani ya Simba na kufunga jumla ya mabao tisa na kutoa asisti 15 katika michuano hiyo.

Miquissone naye amerejea Simba baada ya kushindwa maisha ya uarabuni.

Wakati huo Miquissone aliuzwa Dola 1,000,000 ambazo ni zaidi ya Sh2.3 Bilioni na mshahara wa Dola 34,000 kwa mwezi sawa na Sh80 milioni.

MSUVA - YANGA

Mashabiki wa Yanga waliumia mioyo, Julai 29, 2017 baada ya kuuzwa kwa aliyekuwa Staa wao kwa wakati huo, Simon Msuva kwa Defaa El Jadida ya Morocco.

Msuva wakati huo alikuwa ametoka kuwa mfungaji bora wa ligi akicheka na nyavu mara 14 na kuwapa furaha mashabiki wa Yanga lakini taarifa ya kuuzwa kwake iliwaumiza kimya kimya baada ya kushindwa kumbakisha.

Msuva aliuzwa kwa Dolla 150,000, ambazo ni sawa na Sh 366 milioni za kibongo.

OKWI - SIMBA

Julai 10, 2015 ilikuwa siku ngumu kwa mashabiki wa Simba baada ya kuuzwa rasmi kwa aliyekuwa staa wao kwa wakati huo, Winga Mganda Emmanuel Okwi.

Wakati Okwi yuko moto katika ubora wake na mashabiki wa Simba wakipenda kuendelea kuwa naye kikosini, Simba ilikubali ofa ya kumuuza nchini Denmark katika timu ya Sonderjyske baada ya kuwekewa mkwanja wa maana mezani.

Wakati huo Okwi aliuzwa kwa Dola 110,000 ambazo ni sawa na Sh 268 milioni za Kibongo fedha nyingi sana kwa wakati huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live