Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna aliye salama Ligi Kuu Bara

Mtibwa Ligi Kuu Hakuna aliye salama Ligi Kuu Bara

Wed, 15 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara inakwenda ukingoni huku ikibaki kati ya michezo mitatu hadi minne kwa baadhi ya timu ili kumaliza msimu huu, lakini mbali na bingwa kupatikana ambaye ni Yanga aliyebeba mara tatu mfululizo, kuna vita kubwa ipo katika nafasi ya kushuka daraja.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kuanzia timu inayoshika nafasi ya tano hadi ya 16 inayoburuza mkia hakuna yenye uhakika wa kubaki kutokana na pointi zinavyopishana jambo linalozidi kuongeza ushindani kwenye michezo iliyobaki.

Mtibwa Sugar inayoburuza mkia na pointi 20 ikiwa itashinda mechi tatu zilizobaki itafikisha alama 29 ambazo zitaitoa mkiani hadi nafasi ya 13, ambapo zitaifanya kupata nafasi ya kujitetea kwenye michezo ya kuwania kubaki maarufu kama mchujo (play-off).

Mtibwa itaanza na Namungo FC kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Mei 20, kisha kumalizia mechi mbili ugenini ikienda kwa Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma Mei 25 na kuifuata Ihefu katika dimba la CCM Liti mjini Singida, Mei 28.

Mchezo wa kwanza Mtibwa ilichapwa bao 1-0 na Namungo, Desemba 7, mwaka jana na ilipokutana na Mashujaa ilishinda mabao 2-1, Desemba 19 kisha kuchapwa 3-2 na Ihefu Februari 12, mwaka huu jambo ambalo haitakuwa rahisi zaidi kwao.

Geita Gold iliyopo nafasi ya 15 na pointi 25 ikiwa itashinda michezo mitatu itaifikisha 34 zitakazoisogeza hadi nafasi ya tano japo itategemea na matokeo ya, Tanzania Prisons, KMC, Ihefu, Namungo JKT TZ na Kagera Sugar zilizopo juu zaidi.

Michezo ya Geita iliyosalia ni dhidi ya Simba Mei 21 Uwanja wa Azam Complex na Singida Fountain Gate Mei 25, Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kisha kuhitimisha msimu kwa kupambana na Azam FC Mei 28 kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Nyankumbu.

Mchezo wa kwanza Geita ilichapwa bao 1-0 na Simba, Februari 12, mwaka huu na wakati ilipokutana na Singida iliichapa 1-0, Desemba 21, mwaka jana kisha ilipocheza dhidi ya Azam Uwanja wa Azam Complex ilifungwa 2-1, Februari 16, mwaka huu.

Tabora United na Mashujaa zilizopo nafasi ya 14 na 13 ambazo zina uwezekano wa kucheza mtoano ili kusalia katika Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao kwa michezo iliyosalia zinaweza kutoka zilipo na kusogea juu ikiwa zitachanga vyema karata zao.

Tabora na Mashujaa zenye pointi 26 kila mmoja ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa zikiwa zitashinda michezo yao mitatu iliyobaki zitafikisha pointi 35 na kusogea hadi nafasi ya tano ikiwa timu nyingine za juu zitakuwa na matokeo mabovu.

Michezo iliyobaki kwa Tabora ni dhidi ya Ihefu Mei 20, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kucheza mechi zote mbili zilizobaki ugenini ikianza na mabingwa wapya wa Ligi Yanga Mei 25 kisha kuifuata Namungo FC Mei 28, Uwanja wa Majaliwa.

Kwa upande wa Mashujaa itaanza ugenini na Tanzania Prisons inayowania nafasi ya nne Mei 20, na kuikaribisha Mtibwa Sugar Mei 25 Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma kisha kuhitimisha msimu kwa kucheza na Dodoma Jiji Mei 28 ikiwa uwanja huo huo.

Singida iliyopo nafasi ya 12 na pointi 30 ikiwa itashinda michezo mitatu iliyobaki itamaliza nafasi ya nne ikitegemea na matokeo ya wengine sawa na ilivyokuwa pia kwa Dodoma Jiji yenye pointi 30 ingawa imebakisha mechi nne kuhitimisha msimu.

Michezo iliyobaki kwa Singida ni dhidi ya KMC leo kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Geita Gold Mei 25, Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na kuhitimisha na Kagera Sugar uwanja huo huo Mei 28 huku Dodoma ikianza na Simba Mei 17, Uwanja wa Jamhuri.

Baada ya hapo Dodoma itaikaribisha Yanga Mei 22 na kuifuata Ihefu Mei 25, Uwanja wa CCM Liti Singida kisha kuhitimisha msimu kwa kupamba dhidi ya Mashujaa ambao mechi yao ya kwanza ilimalizika kwa kufungana bao 1-1, Februari 11, mwaka huu.

Namungo, JKT Tanzania na Kagera Sugar zilizopo nafasi ya nane, tisa na 10 zote zina pointi 31 ila zikitofautiana tu kwa mabao ya kufunga na kufungwa na endapo zitashinda michezo yao mitatu iliyobaki zitafikisha 39 na kujiweka maeneo mazuri.

Namungo iliyopo ya nane itacheza na Mtibwa Sugar Mei 20, Uwanja wa Manungu Complex kisha kumalizia mechi mbili ikiwa nyumbani ikianza kwa kuialika Tanzania Prisons Mei 25, na kucheza na Tabora United Mei 28, Uwanja wa Majaliwa Ruangwa.

JKT inayoshika nafasi ya tisa itacheza na Azam Mei 20, Uwanja Meja Isamuhyo, kisha kuifuata Coastal Union Mei 25 Uwanja wa Mkwakwani na kumaliza msimu kwa kucheza na Simba Mei 28 huku ikikumbuka kuchapwa mechi ya kwanza bao 1-0, Februari 15, mwaka huu.

Kwa upande wa Kagera Sugar itaialika Coastal Union Mei 21, Uwanja wa Kaitaba na baaada ya hapo itaifuata Azam FC Mei 25, Uwanja wa Azam Complex kisha kumaliza ugenini tena kwa kucheza na Singida Fountain Gate Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Coastal Union iliyopo nafasi ya nne na pointi 38 itakabiliwa na upinzani mkali wa kusaka nafasi ya nne kwa kucheza dhidi ya Kagera Mei 21, Uwanja wa Kaitaba na kuikaribisha JKT Tanzania Uwanja wa Mkwakwani Mei 25 kisha kumaliza na KMC Mei 28.

KMC iliyopo nafasi ya sita na pointi 33 kama ilivyokuwa Prisons iliyopo ya tano ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa zote zina uwezo wa kumaliza nafasi ya nne ikiwa zitapata matokeo mazuri jambo linaloongeza ushindani baina yao.

Michezo mitatu iliyobaki kwa KMC ni dhidi ya Singida FG leo Uwanja wa Azam Complex, kucheza na Simba Mei 25 ugenini kama itakavyoifuata Coastal Union mchezo wa mwisho Uwanja wa Mkwakwani Mei 28, zikiwa zote zinawania kumaliza nafasi nne za juu.

Prisons itacheza na Mashujaa Mei 20 Uwanja wa Sokoine kisha kuifuata Namungo Mei 25 na kumalizia na mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga ugenini pia Mei 28 ambao mechi yao ya kwanza iliyopigwa jijini Mbeya ilichapwa mabao 2-1, Februari 11, mwaka huu.

Ihefu iliyopo nafasi ya saba na pointi 32 ikiwa itashinda michezo mitatu itafikisha 41 ambazo zitawaweka sehemu nzuri japo itategemea na matokeo ya timu nyingine huku ikianza ugenini na Tabora United Mei 20, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Baada ya hapo itamalizia michezo yake miwili iliyobaki ikiwa Uwanja wa CCM Liti Singida kwa kuikaribisha Dodoma Jiji Mei 25 kisha kuhitimisha msimu kwa kucheza na Mtibwa Sugar ambapo mechi ya kwanza ilishinda ugenini 3-2, Februari 12, mwaka huu.

KAULI ZA MAKOCHA Kocha Mkuu wa Tabora United, Masoud Djuma alisema ushindani umekuwa ni mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu jambo ambalo limekuwa likitoa presha zaidi kuanzia kwenye benchi la ufundi hadi wachezaji wenyewe katika kila mchezo husika.

"Timu hazijapishana pointi nyingi ndio maana unaweza ukashinda mchezo mmoja tu ukatoka nafasi ya chini na kukusogeza juu zaidi, tunaendelea kupambana kwa sababu ukiangalia tulipo sio sehemu salama na sitaki kuona tunarudi tulikotoka tena."

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Geita Gold, Denis Kitambi alisema shida pekee inayomuumiza na anayoendelea kuifanyia kazi katika michezo mitatu iliyobaki ni kuangalia namna bora ya kufunga zaidi mabao kwani safu ya ushambuliaji imekuwa butu.

"Mshambuliaji siku zote huwa hafundishwi kufunga lakini tunaendelea kuangalia namna bora ya kuwatengeneza kisaikolojia kwa sababu nafasi zinatengenezwa ila utumiaji wake ndio umekuwa changamoto hivyo tunaendelea kuboresha eneo hilo."

Tanzania Prisons inayonolewa na Kocha, Ahmed Ally ambayo haijaonja ushindi katika michezo minane mfululizo, alisema hata kwa upande wake anashindwa kuelewa shida iliyopo japo amegundua wachezaji wanacheza kama vile tayari wameumaliza msimu.

Chanzo: Mwanaspoti