Klabu ya Chelsea inadaiwa kuwa kwenye mazungumzo na baadhi ya timu za Saudi Arabia juu ya uwezekano wa kumuuza winga wao Hakim Ziyech katika dirisha hili baada ya dili lake la kujiunga na Al Nassr ya nchini humo kufeli.
Ziyech ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani, amekuwa akihitaji kuondoka Chelsea tangu dirisha lililopita la majira ya baridi (Dirisha Dogo).
Kuelekea maandalizi ya msimu ujao, Ziyech hajajumuishwa kwenye kikosi cha Chelsea na ameambiwa kuwa atafute timu atakayojiunga nayo kwani kocha Mauricio Pochettino hana mpango naye.
Licha ya kufeli vipimo vya afya kwa mara ya kwanza, bado taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Al Nassr wanahitaji kumsajili katika dirisha hili na kuna mazungumzo yanayoendelea baina yao na matajiri hao wa London.
Mkataba wa sasa wa staa huyu wa Morocco unatarajiwa kumalizika mwaka 2025. Msimu uliopita alicheza mechi 24 za michuano yote.
Ziyech alipata kunukuliwa akishangazwa na tukio lile la kufeli vipimo vya afya akidai kwamba kulikuwa na mapichapicha yamefanyika ili kumkwamisha katika kukamilisha dili lake hilo.
Ziyech alikuwa moto kwelikweli wakati anakipiga Ajax ambayo alikuwa miongoni mwa nyota walioiwezesha kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019 kabla ya kutolewa na Tottenham.
Alishinda kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea mwaka 2021.