Wataalamu wa mambo ya mahusiano wanaeleza kuwa baada ya wanandoa au wapenzi kuachana hakuna kinachoweza kumuumiza mmoja kama kumuona mwenzake akifurahia maisha na mke au mume mpya.
Wakati mwingine hali hii inatokea hata katika maisha ya soka. Ni pale mchezaji anapotoka timu moja kwenda nyingine na kufanikiwa kuliko alikotoka. Hilo limetokea Ruvu Shooting ambayo waliponea tundu la sindano kushuka daraja wakamtimua beki mzoefu Ligi Kuu, Haji Mwinyi ambaye alitimkia Zanzibar kwenye timu ya KMKM ambayo ilimkuza na kutwaa taji la ligi.
Katika mahojiano na beki huyo namba tatu aliyekipiga pia Yanga ambaye ametwaa ubingwa Zanzibar akiwa na KMKM na kufunguka mambo kibao huku akiwataja waajiri wake wa zamani.
NAMNA ALIVYOTUA YANGA
“2015 nikiwa na KMKM tulishiriki mashindano ya Kagame ambayo yalishirikisha klabu kubwa za Bara Simba na Yanga ndiyo yalinitoa Zanzibar,” anasema Haji
“(kocha) Hans van Pluijm ndiye aliyekiona kipaji changu kwenye mchezo dhidi yao sikumbuki vizuri matokeo, lakini baada ya mchezo aliniita na kuniambia najua kukaba na kutengeneza mashambulizi siku hiyo nilifurahi sana nikajua sifa hizo zimeishia hapo.”
Anasema baada ya mashindano kabla hajarudi Zanzibar alipata taarifa za kuhusishwa kutua Yanga jambo ambalo hakutaka kulichelewesha na msimu huohuo alijiunga na kutwaa mataji mawili mfululizo.
HAKUNA KAMA MIMI YANGA
Ufalme wake uliisha baada ya Gadiel Michael kutua Yanga akitokea Azam aliyechukua nafasi na kumuweka benchi na hapo ulikuwa mwisho wake.
“Niliondoka Yanga kwa sababu sikuwa chaguo la mwalimu aliyekuwepo, sio kwamba nilizidiwa uwezo na aliyekuwa anapata nafasi. Nina uwezo najiamini sana na nina imani kuwa tangu nimeondoka sijawahi kuona aliyeziba pengo langu,” anasema.
“Mpira ni mchezo wa wazi unachezwa kila mmoja anaona. Yanga hawajawahi kupata beki kama mimi tangu nimeondoka nimekuwa nikiwafuatilia, sasa wamesajili nawapa muda ila sidhani kama watafikia uwezo wangu.”
KUTOISAHAU SIMBA
Beki huyo wa zamani wa Yanga amefunguka tukio baya ambalo lilimuumiza, huku akitaja mchezo wa watani Simba na Yanga kuwa ilikuwa mechi ya Ligi Simba walipata kadi nyekundu na kubaki pungufu lakini bado waliifunga Yanga. “Sikumbuki msimu gani ila nakumbuka ulikuwa mchezo wa ligi na Jonas Mkude alipewa kadi nyekundu, lakini upungufu wao haukuwa kikwazo kwani walitufunga. Niliumia sana tulikuwa tumeahidiwa pesa nyingi,” anasema.
CHANGAMOTO ALGERIA
Haji amefunguka changamoto walizokutana nazo akiwa na Yanga nchini Algeria ambapo anasema: “Nchi tuliyokutana na changamoto ambazo sitazisahau kwenye maisha yangu ya soka ni Algeria kwanitutiliwa dawa vyumbani ambazo zilikuwa maalumu kwa ajili ya kupunguza nguvu,” anasema Haji.
“Ukiachana na hilo pia marefa walikuwa hawapo pamoja na sisi. Kila tulipokuwa tunaenda kucheza tulikuwa tunakutana na figisu.”
BILA YANGA HAKUNA HAJI
Chini ya Pluijm, Haji alikuwa beki bora na wa kutumainiwa Yanga, lakini kuondoka kwa kocha huyo kulifuta ubora wake na kuanza kusotea namba kikosi cha kwanza.
“Achana na mimi kukosa namba kikosini hiyo ni sifa ndogo kwangu kwani nakiri bila Yanga na Pluijm nisingefahamika. Nimetambulika sehemu nyingi kutokana na Yanga.Kipaji changu kimekubaliwa na wengi kutokana na mabingwa hao wa kihistoria, najivunia kucheza kwenye timu hiyo,” anasema.
YANGA BUANA
Pamoja na kukiri kuwa Yanga ndio iliyombeba, beki huyo amefunguka kuwa alipotupiwa virago na timu hiyo alijisikia vibaya, lakini hakukata tamaa.
“Kuondoka Yanga hakuna vitu vilivyopungua. Hali hiyo imenionyesha njia ya kuzidi kujituma na kupambania malengo yangu, japo niliachwa kipindi ambacho sikutarajia naamini katika kipaji nitafanya vizuri zaidi nikipewa nafasi kwenye timu nyingine ya Ligi Kuu,” anasema.
PLUIJM KOCHA WA MPIRA
Pluijm ni kocha aliyeweka rekodi nzuri Yanga akiipa ubingwa misimu mitatu mfululizo 2014/ 2015, 2015/ 2016 na 2016/ 2017 na aliifanya kucheza kwa uelewano na kuchukua ubingwa kirahisi.
Pamoja na kuchukua ubingwa aliiwezesha kushiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku pia akichukua Kombe la ASFC.
Hakuna shaka ubora wa Pluijm haukutakiwa kupingwa wala kuhojiwa na nyota huyo wa zamani wa klabu hiyo anasema kuwa ndiye kocha wake bora kwenye Ligi Kuu Bara.
“Pluijm ni kocha wangu bora na ufundishaji wake hakuna mchezaji ambaye alikuwa hauelewi. Alikuwa anatoa nafasi kwa kila mtu na ndio maana alikuwa na mafanikio makubwa,” anasema Haji.
YANGA YAMPOTEZEA MCHUMBA
Umaarufu una faida na hasara hayo yamethibitishwa na beki huyo ambaye anaweka wazi kuwa alijiunga na Yanga akiwa na mchumba na mapenzi yalinoga zaidi akiwa na timu hiyo kubwa. “Mchumba sikumpata Yanga nilikuwa naye tu, lakini tumeshagombana kama miezi mitatu hivi ila kwa sasa kila mtu na hamsini zake vijana wanasema. Naweza kusema kwa sababu sina timu ya kucheza na alizowea kuona napambana na napata umaarufu,” anasema.
YANGA ACHA KABISA
Kuna timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, lakini ni timu mbili tu zinazotajwa midomoni mwa watu na kufuatiliwa kwa ukaribu - Simba na Yanga na wachezaji wengi kutoka timu nyingine wamekuwa wakitamani kuzichezea.
Haji anasema timu hizo ukongwe wao na mafanikio ya kujizolea mashabiki wengi ni kitu pekee kinachozibeba ikiwa ni pamoja na rekodi za mataji mengi.
“Utofauti wa Yanga na timu nyingine upo kwa sababu kwanza ni timu kongwe ina mashabiki wengi na pia timu nilizocheza haziwezi kufanana na timu kubwa hizi nyingine zina changamoto nyingi sana,” anasema.
ZIMBABWE ILIMPANDISHA NDEGE
Kama ulijua Haji kapandishwa ndege na Yanga, unajidanganya kwani kumbe alishapanda muda tu kabla hata hajatua Jangwani.
“Siku yangu ya kwanza kupanda ndege nilikuwa timu yangu ya zamani ya Zanzibar ambayo ipo Ligi Kuu Chuoni FC tulikuwa washindi wa pili tukaenda kucheza (mashindano) Shirikisho (Afrika) Zimbabwe na timu inaitwa Highlanders,” anasema.
“Baada ya kupata nafasi hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda ndege. Niliogopa sana mawimbi ya juu, nilitoka jasho na juu kuna ubaridi lakini nilipata joto,” anasema.
CANNAVARO ATIA NENO
Akimzungumzia Haji, beki mstaafu wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anasema: “Hakuna Mzanzibari mzembe kwenye soka ni mji ambao una vipaji vikubwa. Mwinyi (Haji) alikuwa mchezaji mzuri mwenye kipaji, alidumu ndani ya Yanga kwa misimu miwili kutokana na ubora aliokuwa anauonyesha.
“Najivunia kucheza naye kwenye kikosi kimoja. Kipindi nipo Yanga tulikuwa na safu bora ya ulinz.”
PLUIJM: HAJI NI BORA
Kocha Pluijm anasema Haji ni chaguo lake, ni mchezaji ambaye alimpendekeza kwa viongozi ili asajiliwe sambamba na na Oscar Joshua ambaye alitumika muda mrefu.
“Ni moja ya wachezaji ambaye nimemtumia ndani ya misimu miwili mfululizo akiwa hana mpinzani. Kutokana na kipaji chake ni mchezaji mzuri japo sijafahamu sasa anacheza wapi,” anasema Pluijm.
“Baada ya kuumia msimu wa tatu alisajiliwa Gadiel Michael ambaye pia aliweza kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza. Sikuwahi kumuweka nje Mwinyi kwa kigezo cha kushuka kiwango, hapana. Alipata shida ndio maana nilimpa nafasi Gadiel naye alinifanyia kazi nzuri.”
HAFIDH: HAJI BEKI
Aliyewahi kuwa meneja wa Yanga, Hafidh Salehe anasema: “Nimekutana na wachezaji wa kila aina kuhusu Mwinyi alikuwa mchezaji mzuri na mwenye nidhamu ya soka.”