Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haikuwa rahisi Twiga Stars kufuzu WAFCON

Twiga Stars Kama Yanga Haikuwa rahisi Twiga Stars kufuzu WAFCON

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hatimaye ile kiu ya Twiga Stars kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) imetimia baada ya juzi kufuzu kwa jumla ya mabao 3-2 dhidi ya Togo ugenini na kufuta unyonge wa miaka 13.

Stars ilifuzu baada ya kuanza vyema mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, Novemba 30 kwa ushindi wa mabao 3-0, mawili yakiwekwa kambani na Opah Clement anayeichezea timu ya Besiktas ya Uturuki na moja wakijifunga wageni na katika marudiano ilifungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Stade De Kegue jijini Lome Togo na kufanya matokeo ya jumla ya mabao 3-2 yaliyoivusha Twiga Stars.

Mwanaspoti inakukumbusha safari ngumu ambayo Twiga Stars imekuwa nayo kuanzia mwaka 2010 hadi leo hii kufuzu Fainali za WAFCON.

Mwaka 2012, Twiga Stars haikuwa kati ya timu za mataifa manane ambayo yalishiriki fainali za WAFCON katika awamu iliyofuata baada ya ile iliyofanyika 2010 Afrika Kusini, ambapo ilikuwa ni mwaka huo fainali hizo zilipofanyika nchini Guinea ya Ikweta.

Timu nane za Afrika ambazo zilipata fursa hiyo zilikuwa ni mwenyeji Guinea ya Ikweta, DR Congo, Ethiopia, Ivory Coast, Nigeria, Senegal na Afrika Kusini ambapo wenyeji walimaliza wakiwa mabingwa.

Harakati za Twiga Stars kufuzu fainali hizo za 2012 zilikwama katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kuwania kufuzu ambapo ilitolewa na Ethiopia baada ya kuchapwa mabao 3-1 katika mechi mbili baina yao.

Katika mechi ya kwanza ugenini, Twiga Stars ilipokea kichapo cha mabao 2-1 na ziliporudiana Dar es Salaam, ikapoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Ikumbukwe katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu, Twiga Stars ilipenya kuingia raundi ya kwanza baada ya kuitupa nje Namibia katika raundi ya awali kwa ushindi mnono wa mabao 7-2, ikishinda mabao 2-0 ugenini na nyumbani ikapata ushindi wa mabao 5-2.

Twiga Stars haikushiriki WAFCON mwaka 2014 wakati fainali hizo zilipofanyika Namibia baada ya kutolewa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kufuzu na timu ya taifa ya wanawake ya Zambia kwa kichapo cha mabao 3-2 katika mechi mbili walizocheza.

Katika mchezo wa kwanza ugenini huko Zambia, Twiga Stars ilichapwa mabao 2-1 na ziliporudiana hapa Dar es Salaam, mchezo ukamalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika mashindano ya kuwania kufuzu WAFCON mwaka 2016, fainali ambazo zilifanyikia Cameroon, Twiga Stars kwa mara nyingine ilikomea katika raundi ya kwanza kwa kutolewa na Zimbabwe ikichapwa mabao 3-2.

Ilianza kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-1 na ilipoenda ugenini ikatoka sare ya bao 1-1

Mwaka 2018, fainali za WAFCON zilifanyika Ghana na Twiga Stars haikuweza kushiriki kwa vile iliondolewa na Zambia katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kuwania kufuzu kwa kanuni ya faida ya mabao ya mengi zaidi ya ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 4-4.

Katika mchezo wa kwanza nyumbani, Twiga Stars ililazimishwa sare ya mabao 3-3 na ziliporudiana ugenini huko Zambia, mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mwaka 2020, kulitokea mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 uliosababisha WAFCON isiwepo na zikaja kufanyika Morocco mwaka 2022 ambazo hata hivyo Twiga Stars haikufuzu.

Twiga Stars ilitupwa nje na Namibia raundi ya kwanza baada ya kufungwa mabao 5-3 katika mechi mbili walizokutana, ikipoteza kwa mabao 2-1 nyumbani na ugenini ikifungwa mabao 3-2.

TIMU 12

Timu 12 kutoka mataifa mbalimbali yatashiriki fainali hizo ambazo ni Morocco, Afrika Kusini, Algeria, Ghana, Botswana, DR Congo, Tunisia, Senegal.

Wengine ni Zambia, Tanzania, Mali na Nigeria ambayo imeshatwaa ubingwa huo mara 11 na ndio timu iliyobeba mara nyingi, ikifanya hivyo mwaka 1991, 1995, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2010, 2014, 2016 na 2018.

Bingwa mtetezi wa mashindano hayo mwaka 2022 ni Afrika Kusini na mshindi wa pili Morocco ambaye ndio mwenyeji wa fainali hizo, Zambia akishika nafasi ya tatu huku Nigeria ikimaliza nafasi ya nne.

MALENGO TU

Ukiachana na figisu walizofanyiwa Twiga nje ya uwanja lakini katika mchezo huo uliovusha Twiga, wadada hao walipambania bendera ya nchi ugenini kila mmoja akijitoa kwa nafasi yake uwanjani.

Twiga iliingia kwenye mchezo huo ikiwaheshimu wapinzani wake na kucheza soka la malengo ya kutaka kufuzu na sio kushinda.

Mbali na kuruhusu mabao hayo lakini safu ya ulinzi chini ya kipa Naijat Abbas ilikuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani licha ya kuonekana kuwepo upungufu eneo la kushoto.

Opah, Stumai Abdallah na Donisia Minja wanaendelea kuonyesha ukomavu wa hali ya juu eneo la ushambuliaji lakini bado kuna shida kwa Aisha Masaka ambaye mechi mbili mfululizo anakosa utulivu langoni mwa mpinzani kwani juzi alibaki na kipa katika dakika ya 45 ya mchezo lakini alishindwa kufunga bao.

HESHIMA

Hii ni heshima kwa Tanzania kwani timu zote za taifa zimefuzu, Taifa Stars ambayo ilifuzu kushiriki fainali za AFCON zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast kwa kutoa sare ya bila kufungana na Algeria ugenini.

Hayo yanaonyesha maendeleo kwa taifa la Tanzania kwa kutoa timu zote kufuzu kwa upande wa wanawake na wanaume zote zikiwa kwebnye kiwango cha hali ya juu.

WASIKIE WENYEWE

Kipa wa JKT Queens na Twiga Stars, Naijat anasema mtaji wa mabao waliopata nyumbani ndio umeisaida timu yao na historia mpya imeandikwa kwa miaka mingi bila ya kushiriki.

“Tunamshukuru Mungu, tumefuzu baada ya miaka mingi, kikubwa tutamsikiliza kocha kwa hatua inayofuata tunajua waliopita sio wabaya tutahakikisha tunafanya vyema.” anasema Naijat.

Beki wa Simba Queens na Twiga Stars, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ anasema mchezo huo ulikuwa mgumu na maelekezo ya kocha wao, Bakari Shime ndio yaliwasaidia kufuzu hatua inayofuata.

“Tumefurahi kufuzu hatua inayofuata, tunaamini tumecheza vizuri ndio maana tumepita kutokana na maelekezo ya kocha licha ya mchezo kuwa mgumu,” anasema Fatma.

Chanzo: Mwanaspoti