Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Habibu Kondo amesema yeye na wachezaji wake wana kazi ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri na kuondoka kwenye nafasi mbaya iliyopo hivi sasa.
Mtibwa Sugar ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 2 baada ya kutoka sare mechi mbili huku ikipoteza michezo mitatu dhidi ya Simba SC, Singida Big Stars na Tanzania Prisons.
Kocha huyo mzawa amesema kukosa uzoefu kwa wachezaji wake ndiko kunachangia washindwe kumudu ushindani uliopo kwenye ligi.
“Tumesajili wachezaji wengi ambao hawana uzoefu na Ligi Kuu, ndio maana tumekuwa tukipata wakati mgumu kwenye mechi zetu lakini nafurahi kuona tunaimarika mechi hadi mechi naamini tutafanya vizuri huko mbele,” amesema Kondo.
Kocha huyo amesema kuanza ligi kwa kukutana na timu kubwa nako kumechangia waanze ligi vibaya kwani vipigo walivyopata kama vimeshusha ari ya upambanaji kwa wachezaji wake.
Amesema yeye kama kocha atajitahidi kutumia taaluma kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake ili waweze kurudi mchezoni na kufanya vizuri kwenye mechi zinazofuata za ligi.
Kondo amesema ligi bado mbichi hivyo nafasi ya kurekebisha makosa yao na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zijazo huko mbele ni mkubwa hivyo anewaomba mashabiki kuondoa hofu.