Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haaland mtegoni usiku wa Ulaya

Haaland Goals EPL.jpeg Haaland mtegoni usiku wa Ulaya

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Erling Haaland ana nafasi ya kumaliza mkosi wa kutofunga katika mechi sita mfululizo za Mashindano ya Ulaya wakati Manchester itakapokuwa ugenini leo usiku kukabiliana na Young Boys ya Uswizi.

Tangu alipofunga katika mchezo wa robo fainali msimu uliopita dhidi ya Bayern Munich ugenini, Aprili 19 mwaka huu ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Haaland hajafunga tena katika mechi tano za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Inter Milan, Red Star Belgrade na RB Leipzig pamoja na ule wa Uefa Super Cup dhidi ya Sevilla.

Katika kipindi hicho ambacho Halaand ameonekana kuwa na ubutu wa kufumania nyavu, kocha Pep Guardiola na Man City yake wameonekana kumtegemea zaidi nyota wa Argentina, Julian Alvarez ambaye katika mabao 13 waliyofunga katika kipindi ambacho Haaland ameshindwa kuonyesha makali, yeye amefumania nyavu mara nne.

Ikiwa inaongoza msimamo wa kundi G na pointi zake sita, Man City itajiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi ya leo kwani itahitaji pointi moja tu katika mechi ya marudiano baina yao ili iweze kujihakikishia siti yake katika hatua inayofuata.

Miamba hiyo ya England inaingia katika mechi ya leo ikiwa na historia ya kibabe ya kutamba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo katika mechi zao 31 zilizopita za hatua hiyo, imepoteza michezo miwili tu.

Marefa wa mechi hiyo wote wanatoka Denmark ambapo wa kati atakuwa ni Morten Krogh atakayesaidiwa na Wollenberg Rasmussen na Steffen Bramsen wwakati mwamuzi wa akiba akipangwa kuwa Peter Kjærsgaard.

Mchezo mwingine kwenye kundi hilo leo, utakuwa huko Leipzig, Ujerumani ambako RB Leizig wataikaribisha Red Star Belgrade wakihitaji ushindi ambao utawafanya wafikishe pointi sita na kuweka hai zaidi matumaini yao ya kutinga hatua ya 16 bora.

Kwingineko, Atletico Madrid itakuwa na nafasi ya kulinda uongozi wa kundi E wakati itakapokuwa ugenini kukabiliana na Celtic na kama watateleza, wanaweza kujikuta wakiipisha Lazio ikiwa itapata ushindi au sare ya ugenini kwa Feyenoord.

Katika kundi F, kinara Newcastle United mwenye pointi nne, atajiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 bora ikiwa atapata ushindi wa nyumbani leo dhidi ya vibonde wa kundi hilo, Borussia Dortmund ambayo inashika mkia ikiwa na pointi moja.

Ushindani mkubwa katika kundi hilo unategemewa kuonekana katika mechi baina ya PSG inayoshika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi tatu dhidi ya AC milan iliyo katika nafasi ya tatu na pointi zake mbili, ambapo mwenyeji PSG anaweza kutanua pengo la pointi baina yake na timu hiyo ya Italia kama atashinda lakini akipoteza maana yake atajikuta akimpisha AC Milan.

Vinara wa kundi H, Barcelona wenye pointi sita, leo watakuwa nyumbani kuwakaribisha Shakhtar Donetski, timu ya nyota wa Kitanzania, Novatus Dismas na mechi nyingine leo katika kundi hilo itakuwa ni baina ya Royal Antwerp dhidi ya FC Porto.

Ratiba Ligi ya Mabingwa Ulaya leo

Barcelona vs Shakhtar Donetsk (Saa 1:45 usiku)

Feyenoord vs Lazio (Saa 1:45 usiku)

Celtic vs Atletico Madrid (Saa 4:00 usiku)

PSG vs AC Milan (Saa 4:00 usiku)

Newcastle United vs Dortmund (Saa 4:00 usiku)

RB Leipzig vs Red Star Belgrade (Saa 4:00 usiku)

Young Boys vs Man City (Saa 4:00 usiku)

Royal Antwerp vs FC Porto (Saa 4:00 usiku)

Chanzo: Mwanaspoti