Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haaland kafanya miaka miwili alichofanya Rooney miaka 16

Haaland X Rooney Haaland kafanya miaka miwili alichofanya Rooney miaka 16

Tue, 27 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hat-trick yake dhidi ya Ipswich Town katika ushindi wa mabao 4-1 wa Manchester City, ilimfanya Erling Braut Haaland afikishe jumla ya hat-trick saba kwake ndani ya mechi 68.

Kwa hat-trick hizi, Haalaand anapanda hadi nafasi ya nane katika orodha ya wakali wa hat-trick nyingi za Ligi Kuu England (EPL)akimfikia Wayne Rooney, nyota wa zamani wa Manchester United na Everton.

Japo rekodi zinaonyesha kwamba Haaland ana misimu mitatu kwenye EPL, lakini msimu wa tatu ndio huu wa 2024/25 ambao amecheza mechi mbili tu.

Hata hivyo, Haaland bado hajafanya maajabu kama ya Alan Shearer, nyota wa zamani wa Southampton, Blackburn Rovers na Newcastle United.

Shearer ambaye jumla ana hat-trck 11, aliwashangaza watu pale alipofunga hat-trick nane ndani ya kipindi cha siku 476 (mwaka mmoja na nusu) kuanzia Novemba 26, 1994 hadi Machi 16, 1996.

Kama hiyo haitoshi, Shearer alitisha zaidi kwa kufunga hat-trick tano ndani ya msimu mmoja wa 1995/96, na kuweka rekodi inayodumu hadi sasa. Alan Shearer ndiye mfungaji bora wa muda wote wa EPL akiweka kambani na mabao 260.

Orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa hat-trick kwenye EPL inaongozwa na Sergio Aguero, nyota wa zamani wa Manchester City. Aguero alicheza Man City kwa misimu 11, kuanzia msimu wa 2011/12 na kuondoka 2021/22.

Haaland ni mchezaji aliyezaliwa kufunga mabao, na anafunga kweli kweli. Akiwa na miaka 24, raia hiyo wa Norway ameshafunga hat-trick saba hadi sasa akiwa na Man City katika mashindano yote.

Kwa ujumla ana hat-trick 22 katika maisha yake ya soka akianzia klabu ya Molde ya kwao Norway, RB Salzburg ya Austria, Borussia Dortmund ya Ujerumani na sasa Man City ya England pamoja na timu yake ya taifa ya Norway.

ATAVUNJA REKODI

Ili amfikie Kun Aguero kileleni, Haaland anadaiwa hat- trick tano tu. Mkataba wake na klabu yake utaisha mwaka 2027 ikiwa na maana bado ana miaka mitatu ndani ya Etihad kama mambo yatakwenda kama yalivyo.

Na endapo ataendelea na moto huu huu alionao sasa, hakuna shaka kabisa kwamba Haaland atakuwa mpiga hat- trick wa muda wote wa EPL. Na kama atadumu kwenye EPL kwa angalau miaka 10, ataweka rekodi ambayo itachukua miaka mingi mno kuifikia.

NI REKODI EPL SIO YA LIGI KIHISTORIA

Ligi ya England ilianza mwaka 1888 ikiitwa English Football League (EFL), ikiwa na madaraja manne; la kwanza, la pili, la tatu na la nne. Daraja la Kwanza ndiyo ilikuwa ligi ya juu zaidi. Hali iliendelea hivyo hadi msimu wa 1991/92.

Ligi zote hizo nne zilikuwa zinasimamiwa na Chama cha Soka England (FA). Kuanzia msimu wa 1992/92 mfumo ukabadilika. Zile timu zilizokuwa Daraja la Kwanza katika msimu wa 1991/92 zikaanzisha ligi mpya, ikaitwa Ligi Kuu England.

Na hiyo ndiyo hii EPL yaani English Premier League, iliyopo hadi sasa. Ligi hii haiko chini ya FA, bali inajitegemea yenyewe ikiendeshwa na kusimamiwa na kampuni yake ya Premier League.

FA ikabaki na yale madaraja matatu yaliyobaki, yaani la pili, la tatu na la nne, katika ligi ile ligi ya EFL.

Kutokana na kujitenga kwa ligi Daraja la Kwanza na kuwa Ligi Kuu, madaraja yaliyobaki nayo yakabadilishwa majina.

Ile ligi ya Daraja la Pili ikaitwa EFL Championship. Ile iliyokuwa Daraja la Tatu ikaitwa EFL League One, na ile iliyokuwa Daraja la Nne ikaitwa EFL League Two.

Kwa hiyo rekodi hizi za Haaland ni kwa Ligi Kuu, yaani ile iliyoanza msimu wa 1992/93, siyo nyuma ya hapo. Endapo ingeanzia nyuma ya hapo, Alan Shearer angelingana na Aguero kwa hat-trick.

Shearer alianza kucheza 1988 katika ile ligi Daraja la Kwanza akiwa na miaka 17. Katika mchezo wake wa kwanza kuanza alifunga hat-trick dhidi ya Arsenal.

Hii ingeingia kwenye hizi hesabu maana yake naye angekuwa nazo 12, lakini bahati mbaya haipo kwenye orodha hii. Kama ilivyoelezwa hapo juu, orodha hii ni ya Ligi Kuu pekee, yaani kuanzia msimu wa 1992/93.

Na katika ligi hii, mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick alikuwa Eric Cantona wa Leeds United, kabla hajahamia Manchester United.

HAT-TRICK NI NINI?

Najua watu wengi tunajua kwamba hat- trick ni kitendo cha mchezaji mmoja kufunga mabao matatu ndani ya mechi moja.

Lakini je, hili neno limetokea wapi hadi kuwa maarufu namna hii?

Tukilichambua neno hilo tutagundua limetokana na kuunganishwa maneno mawili, HAT na TRICK. Hat ni kofia na trick ni mbinu. Kwa hiyo hat-trick ni mbinu ya kofia.

Sasa hii mbinu ya kofia ndiyo inahitaji uchambuzi. Inakuwaje mtu afunge mabao matatu katika mechi halafu iwe mbinu ya kofia? Ni hivi, mpira wa miguu umelichukua neno hili la hat-trick kutoka kwenye mchezo mkongwe zaidi, yaani kriketi.

Kabla ya mpira wa miguu kuwa maarufu, mchezo maarufu na mkubwa zaidi ulikuwa kriketi. Hata sheria za mpira wa miguu, kama ukubwa wa uwanja na idadi ya wachezaji, zimechagizwa na sheria za kriketi.

Kwa hiyo mpira wa miguu ulichukua baadhi ya vitu kutoka mchezo wa kriketi, ikiwemo hat- trick.

Kwenye kriketi, kuna vitu kadhaa ambavyo mchezaji wa timu moja akivifanya anakuwa amemsababishia mchezaji wa timu nyingine kutolewa, yaani inakuwa sawa na kupata kadi nyekundu kwenye mpira wa miguu.

Lakini hatolewi kwa kufanya madhambi kama kwenye mpira, bali kwa kuzidiwa maarifa. Mwaka 1858, mcheza kriketi maarufu wa Uingereza, Heathfield Harman “HH” Stephenson aliwazidi maarifa wachezaji watatu wa timu pinzani, na kuwatoa.

Kitendo kile kiliwafurahisha mashabiki wa timu yake kiasi cha kuchangishana pesa ili kumnunulia kofia. Kuanzia hapo ikawa kama utamaduni kwamba mchezaji atakayewatoa wapinzani watatu anapewa kofia.

Wachezaji wakahamasika sana kutoana uwanjani ili wapate heshima ya kupewa kofia. Kwa hiyo kuwatoa wapinzani watatu ikageuka kuwa mbinu ya kujipatia kofia…na ndiyo ikawa HAT TRICK, yaani mbinu ya kofia.

Neno hilo likawa maarufu na kuhama kutoka kriketi na kwenda kwenye michezo mingine kama mpira, na sasa Haaland anatamba nalo!

Chanzo: Mwanaspoti