Baada ya kikosi cha Manchester City kuiadhibu Nottingham Forest klabu iliyopanda ligi kuu Uingereza msimu huu kwa kichapo cha mabao sita kwa sifuri huku mshambuliaji wao mpya wa Manchester City Erling Haaland akitupia hat-trick yake ya pili mfululizo msimu huu, mshambuliaji huyo hivi sasa ameanza kuzinyemelea rekodi kadhaa katika ligi hiyo na klabu yake ya Manchester City.
Haaland ambaye amefikisha mabao tisa pamoja na kutoa pasi moja ya bao ndani ya mechi tano alizocheza hadi sasa, alifunga hat-trick yake ya kwanza katika mchezo wa mzunguko wa nne dhidi ya Crystal Palace na kufunga tena hat-trick kwenye mchezo uliochezwa siku ya jana Agosti 31, 2022 katika dimba la Etihad na kumpelekea kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick mfululizo kwenye Premier League tangu Sergio Aguero alivyofanaya hivyo msimu wa 2018/19.
Idadi ya mabao tisa ambayo amefunga Haaland hadi sasa ndani ya mechi tano alizocheza inamfanya kuwa mshambuliaji aliyefikisha idadi hiyo kwa haraka zaidi katika historia ya ligi kuu ya Uingereza.
Hii inamfanya mcheza huyo kuanza kuingia kwenye vitabu vya historia ya ligi kuu uingereza mapemaa na kukazia kauli ya kocha wa klabu yake ya Man City Pep Guardiola kuwa mchezaji huyo ataenda kuwa mchezaji mkubwa na wa kukumbukwa ‘Legend’ kwenye klabu hiyo.