Mabao mawili ya Erling Haaland yameisogeza Manchester City karibu zaidi katika kubeba taji la nne mfululizo la Premier League kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Tottenham, ugenini.
Haaland alifunga mabao hayo katika kipindi cha pili kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur, ambapo kikosi cha Pep Guardiola kimerejea kileleni na kuishusha Arsenal ambapo sasa tofauti yao ni pointi mbili huku zikibakiza mechi moja kumaliza msimu.
Katika mchezo huo, makipa wa pande zote mbili walifanya kazi yao vizuri katika kuzuia kabla ya Man City kutumia nafasi mbili za Haaland kufunga.
City walionekana kuwa na malengo zaidi ya kupata ushindi baada ya kipindi cha pili kuanza walikaribia kupata bao dakika ya 47 baada ya Kipa wa Spurs, Giuglielmo Vicario kuokoa mkwaju mkali wa Kevin De Bruyne.
Hata hivyo, Muitaliano huyo hakuwa na uwezo huo tena kwani City waliandika bao dakika ya 51 lililofungwa na Haaland kupitia pasi ya De Bruyne.
Spurs walipaa nafasi nzuri ya kusawazisha baada ya Brennan Johnson kuinasa pasi ya Manuel Akanji na kumwachia Heung-Min Son, ambaye juhudi zake zilizuiwa na kipa wa Man City, Stefan Ortega.
Dakika ya 90+1 Haaland akahitimisha ushindi huo kwa mkwaju wa penalti baada ya Pedro Porro kumchezea vibaya Jeremy Doku. Hilo ni bao la 27 kwa Haaland akiwa kinara akielekea kutetea tuzo yake ya ufungaji bora.
City inahitaji ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya West Ham United ili kutetea ubingwa wao, huku Arsenal ambayo nayo siku hiyo itacheza dhidi ya Everton, ikiiombea City ipate hata sare huku yenyewe ishinde na kuwa mabingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani hivi sasa inawabeba ikiwa tofauti ni bao moja.
Kwa sasa Man City ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 88, Arsenal inafuatia na pointi 86, zote zimecheza mechi 37, bado moja kila upande kuhitimisha msimu wa 2023-2024.