Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HISIA ZANGU: Mambo mawili tunayomkosea Fei Toto

Mayele Feitoto Yanga Mayele na Fei Toto

Sun, 8 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Na baada ya Feisal Salum ‘Fey Toto’ kuzikonga nyoyo za mashabiki wa Jangwani juzi kuna kauli nikazisikia kutoka kwa mashabiki. Wakati mwingine inakwenda mbali zaidi na inakuwa ni kauli za mashabiki wa pande zote nchini. Wale wa timu yake na wale wa wapinzani wao, Simba.

Kauli ya kwanza inanichekesha na ningependa tusaidiane kufumbuana macho. Kwamba Yanga wanapaswa kumlipa pesa nyingi Feisal kwa sababu amekuwa na mchango sawa na wachezaji wengi wa kigeni wanaocheza nchini hasa wale wa klabu yake.

Kuhusu suala la mchango ni kweli. Naambiwa kwamba mpaka sasa Feisal ameichangia Yanga pointi kumi kutokana na mabao yake kuamua mechi.

Wakati mwingine mabao yake yanakuwa ya muhimu zaidi labda pengine kuliko ya Fiston Mayele ambaye amekuwa akionea kwa kufunga mabao mengi ndani ya mechi moja msimu huu.

Feisal amekuwa akifunga yale mabao ambayo yakiihakikishia Yanga pointi tatu. Tangu kocha Nabi amempeleke eneo la mbele akimtoa chiniamekuwa akifunga kadri anavyojisikia. Amempunguzia majukumu Mayele pengine kuliko washambuliaji wengine walivyompunguzia majukumu Mayele.

Na turudi katika suala la maslahi. Nawashangaa kidogo mashabiki. Hili sio tatizo la Yanga. Ni tatizo la Feisal na watu wake. Ni suala la menejimenti yake au mtu anayemsimamia ama namna ambavyo yeye mwenyewe anajisimamia.

Wachezaji wetu mara nyingi wanaishia kulalamika lakini hawajui njia za kupita kwa ajili ya kudai maslahi yao. Narudia kusema kwamba wengi huwa wanageuzwa kuwa mashabiki wa hizi klabu badala ya kugeuka kuwa wafanyakazi wa hizi klabu.

Wachezaji wa kigeni wameweka ukuta kati yao na klabu pindi linapokuja suala la maslahi yao. Wanajua umuhimu wao katika timu, wanapima, wanajiridhisha halafu wanaingia katika vita ya kudai maslahi yao. Bahati nzuri wana watu wa kuwasimamia.

Mfano mzuri wa kwanza ni wa Emmanuel Okwi. Aliletwa nchini na mtu aliyeitwa Geofrey Nyange ‘Kaburu’. Aliletwa akiwa mdogo pale klabuni. Akakulia klabuni na kuibuka staa mkubwa. Wakati analetwa nadhani Mussa Hassan ‘Mgosi’ na kisha Mbwana Samatta walikuwa mastaa katika kikosi cha Msimbazi.

Baadaye walipoondoka Okwi akaibuka kuwa staa mkubwa akaikamata timu. Waulize watu wa Simba jinsi ambavyo Okwi alikuwa imara katika kutetea maslahi yake.

Na licha ya kwamba alikuwa ameletwa na Kaburu bado alikuwa na wakala wake imara kwa ajili ya kutetea maslahi yake.

Ilikuwa mpaka Simba wapate saini ya Okwi ni lazima wahenyeke. Wahakikishe anapata anachotaka na mshahara ambao anautaka.

Tatizo letu wakati mchezaji wa kigeni anafanya haya wachezaji wetu wazawa huwa wanakodoa macho tu. Wanaishia kulalamika kwamba wageni wanalipwa pesa ndefu.

Mwingine ambaye amekuwa mtu imara kusimamia mkataba wake basi ni Clatous Chotta Chama. Wote tunaelewa namna ambavyo hatima ya Chama inakuwa inaelea hewani pindi mkataba wake unapokaribia kumalizika. Hawajui ni namna gani ya kummudu kiurahisi.

Mashabiki wa Simba wakati huu Chama akiwa anaelekea kumaliza mkataba wake huwa wanashika roho zao mkononi kwa sababu hawajui kama ataendelea kubakia katika klabu yao au atakwenda kwa watani zao. Ni tofauti na sasa hivi pale kwa Feisal. Nadhani mashabiki wa Yanga wana asilimia kubwa kwamba atabakia kwao.

Chama pia ana wakala wake. Hajiwakilishi mwenyewe kwa urahisi. Sisi tulio nje mpaka leo hatumjui wakala wa Feisal wala meneja wake. Tunachosubiri ni malalamiko kutoka kwake au kwa mashabiki kwamba anastahili kulipwa sawa na wageni.

Nadhani wachezaji wetu wajifunze kupima umuhimu wao katika klabu zao na kuacha kulalamika kando. Huwa wanapata nafasi ya kukaa chini na kujadili maslahi mapya na klabu zao. Ni wao wenyewe ndio ambao huwa hawatumii nafasi hizi adhimu.

Yanga wapo sahihi. Ni taasisi ambayo inaangalia kwa karibu maslahi yake moja kwa moja. Ingependa kubana matumizi kwa kulipa kiasi kidogo cha pesa kwa wafanyakazi wake kadri inavyowezekana.

Sio tu kwa Feisal ingependa hata kumlipa Aziz Ki shilingi milioni mbili kwa mwezi kama ingewezekana. Ingependa kumlipa Mayele shilingi milioni tatu kwa mwezi kama inawezekana.

Kinachosababisha wawalipe hawa wachezaji pesa nyingi ni kwa sababu kwanza wachezaji wanajua umuhimu wao klabuni lakini pia wanajua namna ya kusimamia maslahi yao ndani ya klabu. Hii ndio tofauti kubwa kati yao na sisi.

Kwa mfano pale Simba ni rahisi tu kwa mchezaji kama Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kujua umuhimu wake klabuni.

Ni lini Simba wanaweza kumpata mlinzi wa kiwango chake kama ghafla akihama zake Simba kwa kushindwana maslahi. Kuna uwezekano Simba wakatumia pesa nyingi maradufu kupata mbadala wake kutoka nje. Kwanini pesa hiyo wasimpe yeye?

Ni kama kesi ya Aishi Manula. Simba kama wangempoteza Aishi si ajabu wangetumia pesa nyingi kusaka mbadala wake pengine kuliko pesa ambayo wangempa Aishi.

Jiulize, ni makipa wangapi wamepita Yanga mpaka wamefikia hatua ya kutulia na Djigui Diarra? Wachezaji wapime umuhimu wao.

Jambo la pili ambalo tunakosea kuhusu Fei ni suala la yeye kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa. Utasikia watu wanaulizana “hivi nani anamsimamia Fei? Inabidi aende nje.” Huwa inachekesha kidogo na watu hawaambiani ukweli kuhusu jambo lake.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, Feisal ana umri wa miaka 24. Januari mwakani atatimiza miaka 25. Ni wazi kwamba Januari 25 itamkuta hapa hapa. Kwenda Ulaya moja kwa moja kucheza ukiwa na miaka 25 ni jambo gumu.

Unaweza kwenda kucheza katika ligi zisizo na ushindani kitu ambacho sio ndoto zetu. Tungependa kumuona mchezaji kama yeye akicheza katika ligi za ushindani. Hata hivyo kwa umri wake ni kama amechelewa.

Mbwana Samatta alikwenda moja kwa moja Ulaya akiwa na umri wa miaka 23 na bahati yake wasifu wake ulikuwa unambeba. Aliondoka akiwa mmoja kati ya wafungaji bora wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika, lakini aliondoka akiwa na wasifu wa kuwa mchezaji bora wa ndani katika soka la Afrika.

Hivi vyote viwili Feisal hana na tayari ameshapitisha miaka miwili mbele ya Samatta. Anaweza kupata dili zuri katika klabu kubwa za Afrika au Asia lakini kwa sasa moja kati ya vitu vya msingi vilivyo mbele yake ni kupata dili zuri ndani ya Yanga au nje ya Yanga. Hili ni muhimu zaidi.

By Edo Kumwembe

Chanzo: www.tanzaniaweb.live