Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HATARI: Azam na jinamizi la makocha

Moallin.jpeg Abdihamid Moallin

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Licha ya Azam FC kunolewa na makocha zaidi ya 15 tangu ilipopanda daraja msimu wa 2008/09, imefanikiwa kutwaa taji moja tu la Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14 tena kwa rekodi ya kufungwa chini ya Mcameroon, Joseph Omog.

Ukiachana na ubingwa wa ligi mwaka 2014, ilifanikiwa pia kutwaa kombe la Kagame mwaka 2015 chini ya Kocha Stewart Hall, raia wa England na mwaka 2018 lilichukuliwa na Kocha Aristica Cioaba raia wa Romania.

Makala hii inakuletea orodha ya makocha 15 waliopita katika timu hiyo na kile walichokifanya kuanzia walipopanda daraja.

MOHAMMED KING (ZANZIBAR)

Nyota huyu wa zamani wa Small Simba, ndiye aliyeipandisha timu hiyo daraja, kutoka Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Ilala hadi kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008-2009. Mara baada ya timu kupanda, uongozi ulifanya mabadiliko ya benchi la ufundi kutokana na kanuni kuwabana na hivyo kumpa majukumu kocha aliyewahi kuinoa Simba, Neider dos Santos.

NEIDER SANTOS (BRAZIL)

Kocha huyo alitua Azam kwa mbwembwe na misimu yake ya awali aliifanikisha timu hiyo kumaliza nafasi ya tisa ikikusanya pointi 26 baada ya kucheza mechi 22, ikiwa imeshinda saba na sare tano, ikipoteza 10.

Hata hivyo, mabosi wa Azam walionekana kutoridhishwa na nafasi waliyofikia kwenye msimamo na kufungashiwa virago na kumleta aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Itamar Amorim.

ITAMAR AMORIN (BRAZIL)

Mbrazili huyo ndiye aliyechukua mikoba ya ndugu yake msimu wa 2009-2010 na kipindi chake alifanya kazi nzuri ya kumaliza ligi kwenye nafasi ya tatu, nafasi tano tofauti na Dos Santos alivyomaliza msimu mmoja kabla yake.

Azam ya Itamar ilimaliza na pointi 33 kutokana na mechi 22, huku ikishinda nane na kupata sare tisa, ikipoteza tano tu, lakini licha ya kupandisha kiwango cha timu kocha huyo mkataba wake ulivunjwa na mikoba kukabidhiwa Hall, wakati lengo la uongozi likiwa ni kupata ubingwa wa Ligi Kuu.

STEWART HALL (ENGLAND)

Ndiye kocha aliyedumu muda mrefu ndani ya Azam FC, kwani, alitoka nayo mwaka 2010 hadi 2012, na kuifanya kuwa tishio kwa Simba na Yanga baada ya kuisaidia kutwaa taji lake la kwanza la Mapinduzi.

Katika vipindi vyake, Azam ilitwaa taji moja tu la ligi na Kombe la Mapinduzi mwaka 2012, baada ya kuichapa Jamhuri ya Zanzibar mabao 3-1.

Msimu wake wa kwanza wa 2010/11 Azam ilishika nafasi ya tatu, lakini ikipata ushindi wa mechi 13 kati ya 22 ilizocheza, ikikusanya pointi nyingi hadi mwisho wa msimu (43) ambazo ni ongezeko la pointi 10 kutoka msimu uliopita. Msimu uliofuata wa 2011/12, Hall aliiwezesha kuweka rekodi binafsi kwa kumaliza msimu nafasi ya pili na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2013.

Katika mechi 26, ilikusanya pointi 56 baada ya kushinda mechi 17 kwenye mechi za kimataifa, Azam ilifika hadi raundi ya pili na kutolewa na FAR Rabat ya Morocco.

Mwisho wa ‘ndoa’ ya Hall na Azam ni baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga, kwenye fainali za Kombe la Kagame 2012 aliyetua timu ya Sofapaka ya Kenya.

BORIS BUNJAK (SERBIA)

Bunjak ndiye aliyebeba mikoba ya Hall, lakini hakuchukua muda mrefu sana kabla ya kutimuliwa baada ya timu kuonekana kuyumba.

Bunjak aliiongoza Azam kwa muda wa miezi isiyozidi miwili kuanzia Agosti 2012 hadi Oktoba, kabla ya Azam kutoa kali ya mwaka kwa kuusitisha mkataba wake wa miaka miwili kisha wakamrejesha Hall kutoka Sofapaka.

Azam ilinufaika na kurejea kwa Hall, kwani ilirudi kwenye kiwango chake msimu wa 2012/13 walipomaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Licha ya kuipa taji la Mapinduzi, Azam ilimfungashia virago kocha huyo baada ya kuchemsha kwenye Kombe la Shirikisho, alipotolewa kwenye raundi ya awali na Ferroviario da Beira ya Msumbiji, lakini muda sio mrefu akapewa kibarua katika kituo cha kukuza soka la vijana cha Kidongo Chekundu kinachodhaminiwa na kampuni inayojihusisha na masuala ya umeme ya Symbion na Sunderland ya Ligi Kuu England.

JOSEPH OMOG (CAMEROON)

Kuondoka kwa Hall kulitoa nafasi kwa Mcameroon Omog kuinoa Azam, akiwa ametokea kuipa ubingwa AC Leopard ya Congo Brazzaville.

Omog alitua Azam huku ikiwa na moto, ikitoka kunyakua taji lao la kwanza la ligi. Kocha huyo aliiongoza Azam kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014, lakini ikaondolewa mashindanoni katika raundi ya awali na El Merreikh ya Sudan.

Kutolewa huko ni kama kuliwachefua mabosi wa Azam, walioamua kuachana naye ikiwa ni baada ya kufanya vibaya pia katika Kombe la Mapinduzi walikoondolewa na KCC ya Kenya. Katika miaka yake miwili ndani ya Azam, Omog aliiongoza mechi 55 zikiwamo 27 za ligi kuu, 19 ya michuano ya Kombe la Kagame, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Mapinduzi na michezo tisa ya kirafiki.

GEORGE NSIMBE (UGANDA)

Mganda huyo maarufu kama ‘George Best’, alipewa mkataba wa muda kuiongoza Azam baada ya kutimuliwa kwa Omog, lakini akashindwa kuisaidia Azam kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, Azam ilimaliza nafasi ya pili kwa mara nyingine tena na kuwafanya mabosi wa Azam kufikiria suala la kumrudisha tena Hall kutoka katika kituo cha kidogo chekundu.

Ikiwa ni mara yake ya tatu, Hall kuinoa timu yao katika mechi za ligi na michuano ya kimataifa, kocha huyo aliisaidia Azam kutwaa taji lao la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame kwa kuifunga Gor Mahia kwenye fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hata hivyo, katika ligi Azam ilishindwa kuonyesha cheche licha ya kuwa chini ya jopo la wataalamu kutoka ulaya kwani, Yanga ilimaliza kwa kishindo mbele yao, huku Azam ikinusurika kupoteza nafasi ya pili.

Kabla ya kumalizika kwa ligi, huku Yanga wakiwa mabingwa, Hall alitangaza kuachana na Azam na kutoa nafasi ya kuletwa kwa kocha, Zeben Hernandez.

ZEBEN HERNANDEZ (HISPANIA)

Kocha huyo alitua Azam akitokea klabu ya daraja la tatu ya CD Santa Ursula na kusaini mkataba wa miaka miwili na kuanza kibarua chake mwanzoni mwa ligi msimu WA 2016/17.

Hernandez ameondoka Azam akiwa ameingoza mechi 17 za ligi na moja ya Ngao ya Jamii na kushinda mechi nane, sare sita na kufungwa mara nne.

ARISTICA CIOABA

Msimu wa 2017/18 kikosi cha Azam hakikufanya vizuri na kiliondolewa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Mtibwa Sugar.Pia ilimaliza Ligi nafasi ya tatu na pointi 45 baada ya kucheza michezo 23.

HANS PLUIJM (UHOLANZ)

Pluijm alidumu msimu mmoja ndani ya kikosi hicho baada ya kuiongoza Azam FC kwenye michezo 25 na kuvuna pointi 50 na alifanikiwa kuipa timu hiyo mataji mawili, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Kombe la Kagame Agosti mwaka jana na Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu.

ABDUL MINGANE (TANZANIA)

Mingange alipokea mikoba ya Pluijm akisaidiana na Idd Nassor ‘Cheche’ kama msaidizi wake na waliiongoza timu hiyo kwa muda wakimalizia msimu aliouacha njiani Mholanzi huyo.

ETIENNE NDAYIRAGIJE (BURUNDI)

Alijiunga Azam FC msimu wa 2019 hakudumu muda mrefu ndani ya kikosi hicho baada ya kupata ofa ya kuinoa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na kuuomba uongozi wa timu kuridhia ombi la Shirikisho la soka Tanzania (TFF) waliokuwa wanamuhitaji awe kocha wa kudumu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

ARISTICA CIOABA (2019–2020)

Chini ya Cioaba imecheza jumla ya mechi 12 ndani ya msimu wa 2019/2020 ilishinda mechi nane na kulazimisha sare moja mbele ya JKT Tanzania kwa kufungana bao 1-1 Uwanja wa Azam Complex imepoteza mechi tatu na ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri. Mechi ya pili ilikuwa dhidi ya KMC Uwanja wa Uhuru na ya tatu ilikuwa dhidi ya Yanga Uwanja wa Azam Complex na zote ilipoteza kwa kufungwa bao mojamoja. Akiwa ndani ya Azam FC, Cioaba jumla alikiongoza kikosi hicho kwenye mechi 50 ambapo alishinda 28, sare 11 na kupoteza 11.

GEORGE LWANDAMINA (ZAMBIA)(2020-2021)

Desemba 13 mwaka huu kutokana na matokeo mabaya aliamua kuchukua uamuzi wa kujiengua mwenyewe kuinoa Azam FC ambapo alijiunga na timu hiyo akichukua nafasi ya Cioaba.

Lwandamina ameiongoza timu ya Azam FC kucheza mechi 38 za ligi kuu bara, nne za kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na nne za kombe la Shirikisho Afrika na ameondoka akiwa ameiongoza timu ya Azam msimu huu kwenye mechi nane za ligi, huku timu hiyo ikishinda michezo mitatu, imefungwa mitatu na kutoka sare miwili.

ABDIHAMID MOALLIN

Januari 25 mwaka huu Azam FC iliingia mkataba wa miaka mitatu na Moallin baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa takribani mwezi mmoja.

Moallin aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC Academi, alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Mzambia, George Lwandamina, Desemba 13 mwaka jana.

Hata hivyo, kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake uongozi wa timu hiyo Agosti 29 ulitangaza rasmi kuachana na raia huyo wa Somalia aliyekulia Marekani kwa kile kilichoonekana kutofurahishwa na mwenendo wa kikosi hicho katika mechi mbili ilizocheza.

Tangu akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi hicho, Januari 25, Moallin ameiongoza Azam kwenye michezo 19 ya Ligi Kuu Bara na ameshinda tisa, sare tano na kufungwa mitano.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz