BARCELONA HISPANIA. BARCELONA imekuwa na vitu vya kushangaza msimu huu, lakini hii ya kumrudisha Mbrazili Dani Alves na mshahara ambao itamlipa kila mwezi, imeshangaza zaidi ya yote katika zama hizi za ‘hapendwi mtu, inapendwa pochi.’
Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 38 amerejea Camp Nou kukipiga kwenye kikosi hicho, huku akiwa mchezaji anayelipwa mshahara mdogo zaidi kwenye kikosi cha Blaugrana na ataanza kuitumikia timu hiyo Januari wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Alves, ambaye amekuwa mchezaji huru tangu alipoachana na Sao Paulo kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, amekubali mshahara mdogo zaidi, lakini imeelezwa kwamba atalipwa bonasi nyingine kama vile ushindi watakaopata timu katika kila mechi atakazocheza.
Beki huyo atakuwa kwenye kikosi cha kocha mpya wa Barcelona, Xavi Hernandez, ambaye alikuwa mchezaji mwenzake na walicheza pamoja kwa kipindi cha miaka minane kwenye chama hilo la Nou Camp kuanzia 2008 hadi 2016.
Ripoti inadai kwamba mshahara wa Alves kwa wiki ni Euro 1, ikiwa ni dili la pesa ndogo zaidi kwa Ulaya nzima. Jambo hilo limeshtua hasa kwa Ligi Kuu England ambako timu zimekuwa zikilipa mastaa wake mishahara mikubwa kwelikweli.
Hata hivyo, unataka kujua ni wachezaji gani wanaolipwa pesa kidogo ya mishahara wanaocheza kwenye ligi inayofuatiliwa zaidi ya Ligi Kuu England? Hii hapa orodha ya staa mmoja katika kila klabu, kati ya timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu England msimu huu, ambao mishahara yao ndio midogo zaidi kuliko wengine wote kwenye timu zao
Arsenal - Nuno Tavares (Pauni 27,000 kwa wiki)
Tavares analipwa pungufu ya Pauni 3,000 tu kutoka kiwango kile wanacholipwa makinda mastaa kwenye kikosi cha Arsenal, Bukayo Saka na Emile Smith Rowe kwenye mishahara yao ya kila wiki. Kutokana na hilo, Tavares anakuwa mchezaji anayelipwa mshahara mdogo zaidi kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta, ambaye alinasa saini yake kutoka Benfica kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Aston Villa - Jacob Ramsey (Pauni 15,000 kwa wiki)
Baada ya kukubali dili jipya Februaei mwaka huu, kiungo huyo kinda mwenye kipaji cha hali ya juu, amecheza mechi 10 kati ya 11 ilizocheza Aston Villa msimu huu. Bila ya shaka atakuwa tayari kumshawishi kocha mpya Steven Gerrard na kuendelea kumpanga. Lakini, huko Villa Park, Ramsey ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mdogo kuliko wengine, akipokea Pauni 15,000 kwa wiki.
Brentford - Jan Zamburek (Pauni 3,150 kwa wiki)
Wamepanda Ligi Kuu England na kuwashtua vigogo kama Arsenal na Liverpool na kikosi chao kimekuwa cha kawaida sana. Kwenye kikosi hicho maarufu kama Bees, mchezaji wao anayelipwa mshahara mdogo ni kiungo kinda wa miaka 20, Zamburek. Kinda huyo ni zao kutoka akademia ya Slavia Prague na alitokea kwenye Brentford B na analipwa Pauni 3,150 kwa wiki.
Brighton - Jakub Moder (Pauni 10,000 kwa wiki)
Licha ya kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Poland, Moder ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mdogo zaidi kwenye klabu ya Brighton huko kwenye Ligi Kuu England. Baada ya kuaminika sana na makocha wake hasa kwenye mechi kubwa, Moder mwenye umri wa miaka 22 bila ya shaka atapata dili lenye mkwanja mrefu. Kwa sasa staa huyo analipwa mshahara Pauni 10,000 kwa wiki.
Burnley - Will Norris (Pauni 5,769 kwa wiki)
Chaguo la tatu la kipa kwenye kikosi cha kocha Sean Dyche, Norris amecheza mechi tatu tu katika kipindi cha miezi 18 aliyodumu na kikosi hicho cha Turf Moor, Burnley. Kutokana na hilo na kiwango cha mshahara anaolipwa hilo linaeleweka, ambapo staa huyo ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mdogo kwenye kikosi hicho, akipokea Pauni 5,769 kwa wiki.
Chelsea - Marcus Bettinelli (Pauni 35,000 kwa wiki)
Alinaswa kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, staa huyo aliyekulia kwenye kikosi cha Chelsea, ameonyesha umahiri mkubwa kwenye eneo la kipa. Huko, Stamford Bridge, Bettinelli -ambaye ni ngumu kupata nafasi kwenye kikosi hicho cha The Blues ndiye anayelipwa mshahara mdogo zaidi, Pauni 35,000 kwa wiki.
Crystal Palace - Remi Matthews (Pauni 4,700 kwa wiki)
Kipa huyo wa zamani wa Sunderland, Matthews ni chaguo la tatu kwenye kikosi cha Crystal Palace, bado hajacheza mechi yoyote katika kikosi hicho, huku miamba hiyo ya Selhurst Park ilinasa huduma yake Julai mwaka huu. Kwenye kikosi hicho anachochezea staa Wilfried Zaha, ndiye anayelipwa mshahara mdogo kuliko wote, akipokea Pauni 4,700 kwa wiki.
Everton -Anthony Gordon (Pauni 10,000 kwa wiki)
Amekuwa na klabu hiyo ya Goodison Park tangu akiwa na umri wa miaka 11, mzaliwa wa Liverpool, Gordon ndiye mchezaji mwenye mshahara mdogo kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo inayonolewa na Mhispaniola, Rafa Benitez. Analipwa kidogo kuliko hata Jonjoe Kenny na Jarrad Branthwaite. Akiwa na umri wa miaka 20 kwa sasa mshahara wake anaolipwa Everton ni Pauni 10,000 kwa wiki.
Leeds United - Jamie Shackleton (Pauni 17,000 kwa wiki)
Kiungo mwenye kipaji cha juu, Shackleton, 22, ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mdogo zaidi huko Elland Road na ameanza kuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Marcelo Bielsa kitu ambacho kinaweza kumfanya mshahara wake uongezeke. Kwa wakati huu, Jamie mshahara wake anaolipwa na wakali hao wa kupiga pasi uwanjani ni Pauni 17,000 kwa wiki.
Leicester City - Luke Thomas (Pauni 25,000 kwa wiki)
Kinda mwingine anayeibukia kwa kasi kwenye Ligi Kuu England, Luke Thomas, 20. Ameanza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Leicester City, akimpa kocha Brendan Rodgers chaguo muhimu kabisa katika upande wa kushoto. Huko King Power, yeye ndio mwenye mshahara mdogo.