Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gwambina kuvunjwa, mastaa njia panda

Gwambina Mastaa Gwambina kuvunjwa, mastaa njia panda

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya mmiliki wa Gwambina FC kutangaza hadharani kuivunja timu hiyo na kuwataka wachezaji watafute sehemu nyingine, baadhi ya nyota wa klabu hiyo wamefunguka wakisema wameamua kusamehe madeni ya mishahara na posho wanazodai huku wakiambulia nauli za kurudi nyumbani.

Hivi karibuni mmiliki wa timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2018, Alexander Mnyeti ambaye ni Mbunge wa Misungwi, Mwanza, alifikia uamuzi wa kuvunja timu hiyo na kuwaruhusu wachezaji kutafuta maisha sehemu nyingine kwa alichodai ukata na uwepo wa sintofahamu na mamlaka za soka nchini.

Gwambina inayoshiriki Ligi ya Championship inakamata mkia katika orodha ya timu 16 ikiwa na deni la pointi 38, ilicheza michezo 12 pekee kati ya 15 ya raundi ya kwanza, ikishinda mbili, sare moja na kupoteza tisa, huku ikifunga mabao 12 na kufungwa mabao 24. Inadaiwa pointi hizo kibao ikiwa ni adhabu ilizopewa na Bodi ya Ligi kwa makosa mbalimbali ikiwamo ya kutokwenda viwanjani kucheza mechi zao za ligi.

Timu hiyo ilipewa adhabu ya kupokwa pointi 60 (15 kila mchezo) katika michezo minne na Sh 8 milioni (Sh 2 milioni kila mechi) baada ya kutofika uwanjani katika mechi zake dhidi ya African Sports, Mbuni, Fountain Gate na JKT Tanzania.

Mchezaji wa timu hiyo, George Sey aliliambia Mwanaspoti wachezaji walipewa Sh 70,000 ya nauli kurudi makwao, huku wakiamua kutodai malimbikizo ya stahiki zao kwa kuwa hakuna dalili za kulipwa fedha hizo.

Alisema walitaarifiwa na mmoja wa wafanyakazi wa Mnyeti kabla ya dirisha dogo kuwa timu imekufa na watafute maisha kwingine ambapo aliwatumia nauli huku akiwapa matumaini kuwa watajulishwa baada ya kujipanga upya.

“Timu imekufa kweli huyo kiongozi alituambia wana matatizo wamegombana na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kisa uwanja, akatupa nauli Sh 70,000 kwa hiyo wachezaji wote tumeshaondoka, wengi tuliondoka kabla ya dirisha dogo tulikuwa tunasubiria tu nauli,

“Mishahara hatujalipwa ni wababaishaji, tumeamua tu tuwaache kwani mshahara wa mwisho nimelipwa Novemba, 2022. Mazingira yalikuwa mabaya ilishaonekana kuwa timu haitaki hivyo tulimfuata kujua hatma yetu wakatuambia tuondoke mpaka atakapojipanga tena,” alisema George.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo ilipokuwa Ligi Kuu, Kapama Kibadeni alisema anadai takribani Sh 5 milioni za mishahara na posho za mechi tangu akiwa Ligi Kuu, lakini ameamua kusamehe ili kuepuka kuvurugana na mabosi wa timu hiyo kwani bado anatafuta maisha.

“Kulipwa kulikuwa kwa shida sana tangu tunapanda Ligi Kuu tulikuwa tunadai miezi mitatu, mkataba wangu wa awali ilikuwa nalipwa Sh 300,000 kwa mwezi na posho ya mechi Sh 20,000 baadaye ukaboreshwa na kufikia Sh 450,000, lakini mara ya mwisho nimelipwa mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons,”

“Mkataba wangu uliisha Oktoba 2022, tulikuwa tunacheza tu ili kutafuta maisha na tuonekane na timu nyingine, kutokana na hali mbaya ilikuwa najiiba na kwenda kucheza mtaani (ndondo) nipate chochote. Sijawahi kufuatilia madeni, niliamua kusamehe kwa sababu ya kesho yangu ili mtu asikuharibie na kuvurugiana tu,” alisema Kibadeni.

Mwanaspoti limefanya jitihada za kuwatafuta viongozi wa Gwambina kuelezea namna walivyoshughulikia stahiki za wachezaji wao kabla ya kuwaruhusu kuondoka, lakini haikupata ushirikiano huku simu za viongozi hao akiwamo Mwenyekiti Omary Mmasy, katibu Daniel Kirahi na Ofisa Habari, Felix zikiita mara nyingi bila kupokewa.

Kwa upande wa Bodi ya Ligi, kupitia Mtendaji Mkuu wa Bodi, Almasi Kasongo alisema hawana taarifa za Gwambina kujitoa zaidi ya kusikia hewani na wanaendelea kuitambua kama moja ya timu za Ligi ya Championship, ila kwa sasa wanadili na tuhuma walizotoa dhidi yao juu ya uwanja huo.

“Kama bodi hatujapata taarifa ya timu kuvunjwa, tunasikia tu hewani kama wewe, hivyo ni ngumu kusema lolote kwa sasa, ila ni tunaitambua kama timu iliyopo Championship.”

Chanzo: Mwanaspoti