Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gwalala... Kiungo anayetoa tuzo kwa Fei, Aziz Ki

Gwalala Pcn Gwalala... Kiungo anayetoa tuzo kwa Fei, Aziz Ki

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kulikuwa na Mtenje Albano ambaye kwa sasa anakimbiza Dodoma Jiji akifanya vizuri zaidi katika nafasi ya kiungo.

Kwa sasa mashabiki wa Coastal Union huwaambii kitu kuhusu kiungo Greyson Gerald Gwalala, ambaye amekuwa mhimili kwenye eneo la kiungo la timu hiyo.

Ni msimu wake wa pili ndani ya kikosi cha Coastal Union akiwa alisajiliwa kutoka KMKM ya Zanzibar, ubora wake umevivutia vilabu mbalimbali huku Yanga pia ikitajwa.

Kiungo huyo pia amefichua malengo ya Coastal Union msimu huu kuwa kuanzia uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenyewe wanapambana kuhakikisha wanamaliza nafasi nne za juu kitu ambacho amethibitisha kuwa kinawezekana.

17 CHAMA AMEHUSIKA Kila mchezaji anavaa jezi namba mgongoni na zina maana yake kuna ambao wanavaa namba kulingana na idadi ya watoto wa familia yao na wengine kutokana na mapenzi ya wachezaji waliowatangulia.

Kama ilivyo kwa Gwalala ambaye amekiri kuwa anavaa jezi namba 17 kutokana na kuvutiwa na uchezaji wa kiungo wa Simba, Clatous Chama.

"Mimi napenda kuvaa jezi namba 17 kwa sababu ya mapenzi yangu kwa Chama kutokana na aina ya uchezaji wake, hii ni kwa mchezaji wa ligi ya ndani lakini nje ya nchi navutiwa na Kevin De Bruyne kiungo wa Manchester City," Anasema.

LAKI 9 YAMPA MAISHA JAMHURI Mataifa yaliyoendelea wachezaji wanakuzwa kwenye vituo vya michezo na kuuzwa kwa gharama kubwa, kwa upande wa nchi yetu hiyo ni nadra kwani wachezaji wanaibuka kutoka mitaani.

Kama ilivyo kwa Gwalala ambaye amekiri kuwa hadi anapata nafasi ya kucheza ligi ni baada ya kupata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki ya kusaka vipaji.

"Nakumbuka nilikuwa na rafiki yangu anacheza Jamhuri Zanzibar lakini alishindwa kuwashawishi viongozi wake moja kwa moja kuwa ana rafiki yake anaweza mpira alitumia njia ya kuwaaminisha kuwa Ifakara kuna vipaji wanatakiwa kwenda kusaka kwa kucheza mechi ya kirafiki," anasema na kuongeza;

"Uongozi wa Jamhuri ulikubali pendekezo hilo na ndipo walipokuja Ifakara tukacheza mechi ya kirafiki na mimi nilipata bahati ya kuchaguliwa na kusajiliwa kwa dau la Shilingi 900,000, kwa mkataba wa miaka miwili," anasema.

Gwalala anasema msimu wa kwanza alicheza bila malipo ya mshahara lakini kutokana na kipaji chake baada ya kuanza kupata ofa wakaanza kumlipa ili asiondoke bure kikosini mwao.

BINSLUM ALIMPELEKA COASTAL Maisha yake ndani ya kikosi cha Jamhuri yalifika tamati na baadaye alijiunga na KMKM ambayo anakiri kuwa aliichezea kwa mafanikio wakitwaa mataji mawili mfululizo.

"Nikiwa KMKM nilikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza nilicheza kwa mafanikio na kuisaidia timu kutwaa mataji mawili mfululizo ndipo kiongozi wa Coastal Union wakati huo Nassor Binslum alikuwa anafuatilia mechi zetu aliniona na kunileta bara," anasema na kuongeza;

"Ujio wangu ndani ya kikosi cha Coastal nikijiunga kwa miaka miwili na huu ndio msimu wangu wa mwisho ulikuwa na muendelezo mzuri kwani nimepata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na najivunia kuendelea kuimarika," Anasema.

6, 8 POPOTE FRESHI Kuna wachezaji ambao walianza kucheza namba moja uwanjani kuanzia wakiwa na umri mdogo hadi wanaanza mechi za mashindano, lakini kuna wengine wao wameanza kipa, beki au mshambuliaji hadi walipojipata kama anavyo thibitisha Gwalala.

"Nilianza kucheza beki wa kati nikiwa Jamhuri, msimu wa kwanza nilicheza eneo hilo baadaye baada ya timu kubadili kocha aliyekuja aliniona nafaa kucheza kiungo mkabaji.

"Nilipotua KMKM nimecheza namba nane sasa nipo Coastal Union nabadilishwa nafasi kutokana na mahitaji ya kocha amekuwa pia akinitumia nane na sita tangu msimu wangu wa kwanza hadi huu," anasema Gwalala ambaye amekiri kufuata nyayo za baba yake ambaye alicheza mechi za madaraja ya chini akiwa beki namba mbili.

AZIZ KI, FEI TOTO MAFUNDI Ni nadra mchezaji wa ligi moja kumkubali mchezaji mwenzie kwa kumwagia sifa kutokana na uwezo wake kwa Gwalala ni tofauti kwani amekiri kuwa kwa nafasi anayocheza kwa msimu huu kiungo wa Yanga Stephane Aziz Ki na Feisal Salum 'Fei Toto' ni mafundi ambao amewapa tuzo ya msimu.

"Aziz Ki ndiye kinara wa upachikaji mabao msimu huu akifunga mabao 13 (kabla ya mechi ya jana), anafuatiwa na Fei Toto mwenye mabao 11 hawa jamaa kila mmoja anajua anachokifanya msimu huu wao ndio wachezaji bora wa msimu siwezi kutoa tuzo kwa mmoja kwangu ni wote.

"Navutiwa na upambanaji wao kila mmoja ana aina yake ya uchezaji lakini kuna sehemu kila kitu wanafanana kama mashuti nje ya 18 wote ni mafundi wakikulenga manne, mawili watakupata," anasema.

AJIBU KIPAJI CHA SOKA Kila mchezaji ana mchezaji wake wa ndoto ya kutamani kukutana naye au kumuona hasa wale ambao wanacheza ligi moja kiungo huyu amekiri kufurahi kucheza timu moja na Ibrahim Ajibu mchezaji ambaye amemtangulia kwenye soka na alikuwa akimfuatilia.

"Ajibu ni mchezaji mzuri amenitangulia nilikuwa namfuatilia nafurahi kucheza naye timu moja ni mchezaji ambaye amenifanya niendele kuupenda zaidi mpira kwani ni muungwana na mshauri mzuri pale unapotaka kukata tamaa." anasema na kuongeza;

"Hana majivuno ni kiongozi mzuri uwanjani amekuwa na msaada mkubwa kwa Coastal Union akiinua vipaji vya wachezaji wengi kwa kuwaelekeza na kuwapa moyo wa kuamini kuna mafanikio kwenye mpira," anasema.

KAMA SI SOKA BASI FUNDI Kusoma ni kipaji sio kila mwanadamu anaweza kuwa na elimu nzuri darasani hivyo ndivyo alivyosema Gwalala akiweka wazi kuwa kusoma kwake ilikuwa mtihani.

"Mimi sikuwa na kipaji cha kusoma kabisa na wazazi wangu walifahamu hilo na kuamua kuniambia nichague nini cha kufanya na niliomba kusomea ufundi 'mchomelea mageti.

"Nimesoma shule ya msingi Maendeleo na baadaye Sekondari ya Kwilo iliyopo Mahenge Wilaya ya Ulanga, baada ya kuhitimu elimu yangu ya kidato cha nne ufundi nao nikaupotezea na kuamua kujiajiri kwenye soka ambalo ndio linaendesha maisha yangu hadi sasa," anasema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live