Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gusa upigwe, Chama la makundi Qatar

Bruno Fernandes 111.jpeg Bruno Fernandes

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar imeshapita kitambo tu na sasa, mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa wa dunia umeshafikia hatua ya mtoano ya 16 bora.

Hata hivyo, makala haya yanahusu mastaa waliofanya vyema kwenye hatua ya makundi na kuunda Kikosi cha Kwanza matata kabisa kwa mujibu wa mtandao wa takwimu wa WhoScored. Kwenye kikosi hicho kuna mastaa wa mataifa mbalimbali ikiwamo Argentina, England, Brazil, Uholanzi, Ureno, Poland, Morocco na Cameroon. Chama lenyewe hili hapa.

Kipa: Wojciech Szczesny (Poland) - 8.22

Poland ilipenya hatua ya 16 bora na jana Jumapili ilikuwa na kibarua mbele ya Ufaransa kwenye mtoano. Mafanikio ya Poland yamechangiwa zaidi na kipa Wojciech Szczesny, ambaye aliokoa hatari 18, ikiwamo penalti mbili kwenye hatua hiyo ya makundi. Mtandao wa WhoScored umempa alama 8.22 na hivyo anaingia kwenye kikosi hiki, akikaa golini.

Beki wa kulia: Achraf Hakimi (Morocco) - 7.51

Morocco imefanya vizuri sana na kutinga hatua ya 16 bora ikiwa imeongoza kwenye kundi lake mbele ya vigogo Croatia na Ubelgiji, huku staa wao Achraf Hakimi akicheza kwa kiwango bora kabisa na kupewa alama 7.51 na WhoScored. Hakuna mchezaji aliyepiga tako nyingi kumzidi Hakimi (13), huku akiasisti mara moja pia kutokea kwenye beki ya kulia.

Beki wa kati: Jean-Charles Castelletto (Cameroon) - 7.71

Cameroon imetupwa nje ya fainali za Kombe la Dunia 2022 kwenye hatua ya makundi licha ya kuichapa Brazil 1-0 katika mechi yao ya mwisho. Kwenye kikosi hicho cha Simba Wasioshindika kulikuwa na huduma bora kabisa ya beki wa kati Jean-Charles Castelletto, ambaye alinasa mipira njiani mara sita, akifunga na kuasisti. WhoScored imempa alama 7.71.

Beki wa kati: Harry Maguire (England) - 7.43

Kwenye safu ya mabeki ya kikosi hiki, Castelletto atakuwa pacha wa mkali wa England, Harry Maguire, ambaye amekuwa moto kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 na kuwafanya WhoScored kumpa alama 7.43. Maguire amewaziba midomo wabaya wake, akiokoa hatari 12, huku akiwamo kwenye orodha ya wachezaji walioasisti kwenye kikosi cha Three Lions.

Beki wa kushoto: Theo Hernandez (Ufaransa) - 7.98

Theo Hernandez alikuwa chaguo la pili la beki wa kushoto wa Ufaransa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022, lakini baada ya kaka yake, Lucas kuumia goti, alipata nafasi ya moja kwa moja kuingia kwenye kikosi na tangu hapo amekuwa panga pangua hakosi namba. Ubora wake uwanjani umewafanya WhoScored kumpa alama 7.98 na amekuwa akipiga pasi za hatari.

Kiungo mkabaji: Casemiro (Brazil) - 7.89

Kiungo wa Kibrazili, Casemiro amefanikiwa kuingia kwenye kikosi hiki na bao lake pekee alilofunga dhidi ya Uswisi kwenye ushindi wa 1-0 liliisaidia timu hiyo kutinga hatua ya 16 bora. Casemiro, 30 amepiga tako na kunasa mipira njiani mara kadhaa kwenye mechi za makundi na kuwafanya WhoScored kumpa alama 7.89.

Kiungo wa kati: Frenkie de Jong (Uholanzi) - 7.75

Kwenye kikosi hiki, wakati Casemiro akitulia kwenye kiungo ya chini, juu yake atakuwapo Mdachi, Frenkie de Jong - ambaye mavitu yake yamekuwa moto kweli kweli na kuisaidia Uholanzi kutinga hatua ya 16 bora na usiku wa juzi Jumamosi waliitoa Marekani wakiipasua 3-1. De Jong, alipiga tako 11 kwenye hatua ya makundi na WhoScored walimpa alama 7.75.

Kiungo mshambuliaji: Bruno Fernandes (Ureno) - 8.36

Kwenye Namba 10, kikosi hiki kitakuwa na huduma ya kiungo mchezeshaji wa Ureno, Bruno Fernandes, ambaye amepewa alama 8.36 na WhoScored kutokana na makali yake kwenye hatua ya makundi. Staa huyo alihusika kwenye mabao manne kati ya sita iliyofunga Ureno kwenye hatua ya makundi, akifunga mara mbili na kuasisti mara mbili.

Kiungo wa kulia: Antoine Griezmann (Ufaransa) - 7.73

Staa mwingine wa kikosi cha Ufaransa anayepata nafasi kwenye kikosi hiki cha wakali waliofanya kweli kwenye hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar. Antoine Griezmann aliasisti mara moja, huku akipiga pasi muhimu 11. Staa huyo amepiga tako na kunasa mipira njiani mara 10 tofauti. Jambo hili limewafanya WhoScored wampe alama 7.73.

Straika: Kylian Mbappe (Ufaransa) - 7.84

Ufaransa inaonekana kuingiza nyota wengi kwenye kikosi hiki, baada ya Kylian Mbappe kuwa mchezaji watatu wa Les Bleus akiwa kwenye kikosi hicho na mkali huyo ameshafunga mabao matatu kwenye hatua ya makundi na alipiga mashuti 16, huku akitoa mchango mkubwa kwa Ufaransa kutinga 16 bora. WhoScored wamempa alama 7.84

Kiungo kushoto: Lionel Messi (Argentina) - 7.87

Kwenye ile safu ya ushambuliaji, mkali wa Argentina, Lionel Messi atashambulia kutokea wingi ya kushoto. Kwenye hatua ya makundi, Messi alitupia mabao mawili, licha ya kwamba alikosa penalti. Alipiga mashuti 13, pasi muhimu tisa na alikokota mpira mara nane tofauti jambo lililowafanya WhoScored kumpa 7.87.

Chanzo: Mwanaspoti