Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gundogan atundika daluga Kimataifa

Ilkay Gundo Ilkay Gundogan

Wed, 21 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo, Ilkay Gundogan amestaafu soka la kimataifa akiwa na umri wa miaka 33.

Na Mjerumani huyo huenda akarejea kukipiga kwenye timu yake ya zamani ya Manchester City, baada ya kudaiwa mabosi wa Etihad kuzungumza na mawakala wa kiungo huyo ili arudi jijini Manchester.

Barcelona imemwambia Gundogan yupo huru kusikiliza ofa kama anataka kuhama kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Na kiungo huyo aliondoka Man City kwenda kujiunga na Barcelona kwa uhamisho huru kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.

Licha ya kuwa na mkataba hadi 2026, Gundogan aliambiwa Barca haitamzuia endapo kama atapata sehemu ya kuhamia.

Na kinachoelezwa kocha wake wa zamani Pep Guardiola anamhitaji huko Etihad, lakini staa huyo anahusishwa pia na klabu za Uturuki, Fenerbahce na Galatasaray. Man City ilijaribu kumbakiza Gundogan mwaka jana, lakini ilishindwa kufanya hivyo na tangu wakati huo kocha Guardiola alikiri kwamba hawajapa mchezaji wa kurithi buti zake kwenye kikosi hicho cha Etihad.

Gundogan alidai kwamba amechoka na wingi wa mechi za kimataifa na ndio sababu kubwa ya uamuzi wake wa kustaafu. Staa huyo alisema juzi Jumatatu: "Hata kabla ya Euro 2024, nilihisi kuchoka kuanzia mwili na kichwa na ndiyo maana nikaanza kufikiria jambo hili. Mechi za klabu na za kimataifa zimekuwa zikiongezeka tu."

Kiungo huyo wa zamani wa Borussia Dortmund aliichezea Ujerumani mara 82 tangu alipofanya hivyo mara ya kwanza 2011. Gundogan, ambaye aliitumikia Man City kwa miaka saba, alishinda mataji matano ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja.

Hakucheza mechi ya kwanza ya Barcelona kwenye La Liga msimu huu, wakati miamba hiyo ya Nou Camp ilipomenyana na Valencia.

Kocha wa Barca, Hansi Flick alisema sababu za Gundogan kukosa mchezo huo wa ushindi wa mabao 2-1, Jumamosi iliyopita alikuwa na tatizo la kiafya. Mastaa wengine ambao wanaweza kuachwa na Barcelona kwenye dirisha hili ni Raphinha na Ferran Torres.

TAKWIMU ZA GUNDOGAN

BARCA MSIMU WA 2023-24

-Amecheza: Mechi 36

-Ametengeneza: Nafasi 97

-Amepiga: Pasi 2,337

-Amefunga: Mabao 5

-Ametoa: Asisti 9

-Amelala: Takolin 32

-Amegonga: Rafu 15

Chanzo: www.tanzaniaweb.live