Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Guede atua Dar kimya kimya, kuanza kazi leo

Joseph Guede Yangaaaa Guede atua Dar kimya kimya, kuanza kazi leo

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Maandalizi ya Yanga kwa ajili ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika yamepata nguvu baada ya kuwasili kwa nyota mpya, Joseph Guede aliyetua juzi nchini akitokea kwao Ivory Coast kujiunga na kambi iliyopo Avic Town, Kigamboni.

Mshambuliaji huyo ambaye amenaswa na Yanga katika dirisha dogo la usajili akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Tuzlaspor ya Uturuki, alitua usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokewa na maofisa wa timu hiyo kisha kupelekwa Kigamboni ilipo kambi.

Gazeti hili linafahamu kuwa Yanga imefanya ujio wa Guede kuwa wa kimyakimya ili kutomuweka mshambuliaji huyo wa zamani wa FAR Rabat ya Morocco kwenye presha inayoweza kumfanya akose utulivu unaoweza kuathiri kiwango chake.

Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe alikiri kuwasili kwa Guede na kuliambia gazeti hili kuwa tayari ameshaanza programu ambazo timu imeziweka kwa wachezaji.

"Ni kweli mshambuliaji wetu mpya Joseph Guede 'Magoli' ameshawasili nchini na hapa ninapozungumza na wewe yupo na jopo la wataalamu wa afya wa timu akifanyiwa vipimo na tathmini kama ilivyo utaratibu wa timu yetu kuona afya na utimamu wa mwili ukoje kabla ya kuanza mazoezi na wenzake,” alisema Kamwe.

"Vipimo vya kwanza vilikuwa vya afya yake kiujumla ambavyo vililenga kuangalia kama ana tatizo lolote au majeraha na tunamshukuru Mungu yuko salama na leo (jana) atafanyiwa kipimo kingine ambacho hicho ni cha utimamu wa mwili ambacho kitatoa mwelekeo wa aina gani ya mazoezi ambayo benchi la ufundi litaanza nayo kwake."

Kamwe alisema mbali na Guede, wachezaji wengine ambao hawawakuwa na majukumu ya timu za taifa wote wapo Avic Town wakiendelea na programu kama utaratibu ulivyopangwa.

"Timu inaendelea na mazoezi Avic na kipindi hiki cha maandalizi tutacheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo hatutaruhusu mashabiki kwani lengo ni kulipa benchi la ufundi fursa kuona ambacho wamewapa wachezaji kimefanyiwa kazi kwa kiasi gani,” alisema.

Yanga inajiandaa na Ligi Kuu iliyosimama kupisha ushiriki wa timu ya taifa 'Taifa Stars' katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu huko Ivory Coast pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: