Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Guede amkuna Gamondi

Joseph Guedde Kagera.jpeg Guede amkuna Gamondi

Sat, 3 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga inatarajiwa kutua Dar es Salaam ikitokea Mwanza ilipokuwepo tangu jana na kupiga tizi kujiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji itakayopigwa kesho, ikiwa ni saa chache tangu ilipotoka suluhu ugenini na Kagera Sugar, mjini Bukoba, huku kocha mkuu, Miguel Gamondi akikunwa na mwanzo mzuri wa Joseph Guede.

Straika huyo aliyesajiliwa dakika za mwisho za dirisha dogo la usajili, aliingia kipindi cha pili kwenye mchezo wa juzi uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba na kutumika kwa dakika 33 na kocha Gamondi amesema jamaa ana kitu.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Gamondi amesema licha ya kwamba hawakustahili kutoka sare ugenini, lakini kwa vile matokeo yameshatokea hawana jinsi ya kujiandaa kwa mechi nyingine na kueleza wenyeji wao juzi waliamua kucheza mfumo wa kubaki basi na kuwafanya nyota wa timu ya Yanga kushindwa kufanya mambo.

"Nawapa pole mashabiki wa Yanga walioko Kagera na kwingineko kwani walikuja kwa wingi kuiona timu yao lakini hawakuona mpira mzuri kama walivyotarajia kutokana na aina ya uchezaji wa wapinzani wetu. Sisi tulifeli kutengeneza nafasi na kuzitumia, ila tunarudi tukiwa imara katika mchezo ujao ila nje ya yote wachezaji wanatakiwa kuonyesha njaa zaidi ya kutamani matokeo ya ushindi," amesema Miguel aliyeajiriwa mwishoni mwa mwaka jana akitokea Argentina.

Juu ya Guede ambaye hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza tangu sajiliwe na Yanga, kocha Gamondi amesema bado ni mapema mno kwake akitaka apewe muda zaidi, licha ya kukiri ameridhishwa na alivyocheza kwa dakika hizo chache.

"Ni mchezaji mzuri anayetamani kucheza hicho ndicho kinachonifurahisha zaidi kwake, japo bado anahitaji muda wa kuzoea timu ila ameonyesha kitu kizuri kwa mwanzoni," amesema Gamondi.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali, Guende aliingia uwanjani dakika ya 57 akiwa sambamba na straika mwingine, Kennedy Musonda aliyerejea kutoka Afcon 2023 na alionekana mzuri kwenye mipira ya vichwa, huku akiwa mwepesi wa kuachia mipira kwa mwenzake na kujipanga kwa haraka japo ilikuwa mara ya yake ya kwanza.

Nyota huyo na wachezaji wengine wa Yanga wanarudi uwanja wa nyumbani wa Azam Complex, ambapo kesho watakuwa na kibarua mbele ya Dodoma Jiji mechi itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku, huku watetezi hao wakizisaka pointi tatu za kuwarejesha kileleni kwani itaifanya ifikishe pointi 34 na kuiengua Azam inayoongoza kwa sasa.

Mara baada ya mechi ya kesho dhidi ya Dodoma Jiji, watetezi hao watasafiri tena hadi mjini Kigoma kwa ajili ya kuwahi pambano dhidi ya Mashujaa ambao jioni ya jana ilikuwa ikimalizana na Simba kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye muendelezo wa mechi za viporo vya ligi hiyo iliyorejea baada ya kusimama tangu Desemba 23, mwaka jana.

Ligi hiyo ilisimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 inayoendelea Ivory Coast, ambapo Tanzania ilikuwa moja ya nchi 24 zilizoshiriki muichuano hiyo iliyopo hatua ya nusu fainali kwa sasa na fainali ya kupata bingwa mpya ikitarajiwa kupigwa siku ya mwisho, Februari 11.

Chanzo: Mwanaspoti