Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Guede: Wananchi subirini, mbona mtafurahi!

Guede Yanga Ms.jpeg Joseph Guede.

Wed, 28 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede, amesema amefurahi kushusha presha yake na ya mashabiki pia baada ya kufunga bao, hivyo kuahidi kufanya vizuri na kukata kiu yao katika suala la kufunga.

Guede aliyepachika bao la nne katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumamosi iliyopita dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria na kuipeleka timu hiyo hatua ya robo fainali kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikishinda mabao 4-0, amesema kwa sasa yeye na mashabiki pia hawana presha kama ilivyokuwa mwanzo, kwani yeye alikuwa anataka kufunga ili kuonyesha kama ana uwezo huo, na mashabiki walikuwa na wasiwasi naye kama anaweza kufanya hivyo.

Amewaambia waandishi wetu kuwa kwa sasa anaimani mashabiki wa Yanga pamoja na kwamba wanataka kuona anafanya vizuri kwa kufunga katika mechi mbalimbali, lakini hawatokuwa na presha sana kama ilivyokuwa mwanzo kabla hajafunga bao.

“Ilikuwa ni ngumu mchezaji kuingia moja kwa moja kwenye timu na kufanya vizuri, nimepata muda na sasa niko vizuri kuhakikisha nakata kiu ya wanachama na mashabiki ambao wanataka kuona nafunga kwa kila mechi,” amesema Guede.

Ameongeza kuwa kwa sasa atapambana kila anapopewa nafasi ya kucheza kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wa Yanga akiamini atafunga anapopata nafasi ndani ya timu hiyo kwani hatokuwa na wasiwasi tena kwa sababu hata ikitokea akapoteza nafasi mashabiki hawatomchukulia kama walivyokuwa wakimchukulia awali.

Wakati huo huo nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, amesema wanakwenda kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Mabingwa Watetezi, Al Ahly ya Misri bila presha, hivyo wanaweza pia kuweka rekodi nyingine katika bara la Afrika.

Mwamnyeto amesema awali walikuwa na wasiwasi na mechi hiyo kwa sababu walidhani watakwenda kucheza kwa ajili ya kusaka matokeo, lakini kwa sababu wameshapita, ikiwamo wenyeji wao, wanaweza pia kuweka rekodi ya kuifunga Al Ahly nyumbani kwao kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Yanga.

"Mpira ndivyo ulivyo, nani alijua kama tutaifunga CR Belouizdad mabao 4-0, hivi sasa tunamuachia kocha wetu, apange mipango yake na kutupa maelekezo ya jinsi ya kucheza nao, mfumo upi, tucheze vipi, lakini nakuhakikishia patachimbika, mpira utapigwa kwa sababu tutacheza bila presha," amesema nahodha huyo.

Yanga itamaliza mechi yake ya sita Kundi D dhidi ya Al Ahly jijini Cairo, Ijumaa ijayo katika mechi ambayo itaamua timu gani itashika nafasi ya kwanza na ya pili.

Wakati Al Ahly ina pointi tisa, ikiwa kileleni Yanga ina pointi nane, ikiwa nafasi ya pili. Kila mshindi wa kwanza wa kundi atacheza mechi ya robo fainali na mshindi wa pili wa makundi mengine na kuanzia ugenini, huku watakaoshika nafasi ya pili watakumbana na vinara wa makundi ambapo wataanzia nyumbani na kumalizika mechi zao ugenini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live