Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Manchester City, Pep Guardiola amewaambia wachezaji wake nafasi ya kushinda Kombe la Dunia la klabu inatokea mara moja kwenye maisha hivyo wanapaswa kuitumia nafasi hiyo kesho Ijumaa (Desemba 22).
City walifika fainali ya mashindano hayo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Urawa Red Diamonds kwenye mchezo wa nusu fainali Jumanne (Desemba 19). Sasa watacheza na mabingwa wa Amerika Kusini, Fluminense kesho Ijumaa (Desemba 22).
City wanapewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wake wa tano kwa mwaka 2023 lakini Guardiola amewaonya wachezaji wake kutouchukulia poa mchezo huo.
“Tutaenda kula chakula cha usiku pamoja, kutengeneza mazingira kila mmoja kujua umuhimu wa huu mchezo kwa klabu yetu,” amesema Guardiola.
“Kama nilivyosema, kucheza hii fainali unatakiwa kufanya vitu vizuri, kushinda Ligi ya Mabingwa.
“Tumefika hapa ni kombe unaloweza kucheza mara moja kwenye maisha yako yote.
“Kufika hapa ni kitu kizuri kwetu, hatuwezi kuchukulia poa, tunajua tunaweza tusiwe hapa tena.”
Wakati huo huo, City imejulisha Shirikisho la Soka Dunianí (FIFA) kuwa nyota wake; Erling Haaland na Kevin De Bruyne hawatacheza kwenye mchezo dhidi ya Fluminense.
Nyota hao wawili wamesafiri na timu hiyo kwenye mashindano hayo na Jumatatu, De Bruyne alifanya mazoezi na wenzake kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje ya uwanja kwa miezi mitatu akiuguza majeraha yake.
Haaland hajacheza mchezo wowote tangu kipigo cha timu hiyo cha bao 1-0 dhidi ya Aston Villa Desemba 5 na bado hajaanza kufanya mazoezi na wenzake.