Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Guardiola alivyotengeneza kizazi kipya cha makocha wanaotamba Ulaya

Pep Ulaya Guardiola alivyotengeneza kizazi kipya cha makocha wanaotamba Ulaya

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pep Guardiola. Kuna shabiki wa soka ambaye halifahamu jina hilo? Ndiye kocha mkuu wa Manchester City, ambaye katika misimu saba iliyopita, kikosi chake kimeshinda ubingwa wa Ligi Kuu England mara sita.

Ameweka rekodi kwenye Ligi Kuu England ya kushinda ubingwa huo kwa misimu minne mfululizo.

Ametamba na Barcelona, alitamba na Bayern Munich pia kabla ya kutawala kwenye soka la England akiwa na Man City. Hata hivyo, ushawahi kusikia ule msemo wa mtoto wa nyoka ni nyoka? Basi, umahiri huo wa kocha Guardiola - ameripotiwa kuambukiza kwa watu waliowahi kuwa chini yake, ambao pia wamekuwa moto kwelikweli kwenye kazi hiyo ya ukocha, wakifanya maajabu.

Makala haya yanahusu makocha watano kizazi kipya kinachotamba kwa sasa kwenye soka ambao walipita kwenye mikono ya Guardiola.

5.Vincent Kompany (Bayern Munich)

Kocha mpya wa Bayern Munich, Vincent Kompany ni mchezaji wa zamani wa Guardiola. Alikuwa nahodha wake huko Man City na kupata mafanikio makubwa. Alipoondoka Etihad, Kompany alikwenda kuwa kocha huko Anderlecht ya Ubelgiji kabla ya kwenda kuchukua kazi Burnely, ambayo alianza nayo kwenye Championship na kuipandika daraja kucheza Ligi Kuu England.

Bahati mbaya, timu hiyo ilishuka daraja msimu uliopita kabla ya kwenda kuinoa Bayern Munich, akichukua mikoba ya Thomas Tuchel.

4.Enzo Maresca (Chelsea)

Mtaliano huyo alikuwa msaidizi wa Guardiola huko Man City. Lakini, aliinoa pia Parma mwaka 2011 kabla ya msimu uliopita kuwa kwenye kikosi cha Leicester City, alichotamba nacho kwenye Championship, akiipa ubingwa wa ligi hiyo na kufanikiwa kukata tiketi ya kurejea kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wa 2024-25. Hata hivyo, kocha Maresca amebamba dili matata kabisa baada ya kujiunga na Chelsea, ambako amekwenda kurithi mikoba ya Mauricio Pochettino.

3.Erik Ten Hag (Man United)

Wengi wanaweza wasiwe na ufahamu wa jambo hili. Lakini, wakati Guardiola alipokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich, kocha Erik ten Hag alikuwa msaidizi wake, ambapo alikuwa akisimamia Kikosi B cha miamba hiyo ya Allianz Arena. Kwa kipindi hicho, Mdachi huyo alijifunza vitu vya kutosha kutoka kwa Guardiola na kwenda kutamba navyo huko Ajax, alikobeba mataji kibao ya Ligi Kuu Uholanzi kabla ya kupata dili la kwenda kuinoa Manchester United, ambako tayari ameshabeba mataji mawili.

2.Mikel Arteta (Arsenal)

Baada ya kustaafu soka kama mchezaji, Mikel Arteta alinaswa haraka na Guardiola na kwenda kuungana naye kwenye benchi lake la ufundi huko Man City. Baada ya miaka kadhaa ya kujifunza mambo na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England pamoja, Arteta aliondoka kwenye mikono ya Guardiola na kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Arsenal baada ya kuachana na kocha Unai Emery.

Mwanzo wake ulikuwa mgumu huko Emirates, lakini kwa sasa Arteta ameifanya Arsenal kuwa moja ya timu zinazoshindania ubingwa, akimpa shida bosi wake wa zamani.

1.Xabi Alonso (Bayer Leverkusen)

Kiungo wa zamani, Xabi Alonso alicheza chini ya Guardiola wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich.

Sawa, Mhispaniola huyo aliwahi pia kuwa chini ya Jose Mourinho, Carlo Ancelotti na Rafa Benitez kwa kuwataja kwa uchache, lakini kwa kitendo chake cha kuwa chini ya Guardiola kumeongeza ubora wake kwenye benchi la ufundi. Alonso aliongoza Bayer Leverkusen kushinda ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita bila ya kupoteza mechi yoyote msimu mzima.

Chanzo: Mwanaspoti