Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amedai kwamba hana nafasi ya kupoteza alama tena katika Ligi Kuu ya England kwani akifanya hivyo ndoto za kuchukua ubingwa msimu huu zitaishia hapo.
Mabingwa hao watetezi kwa sasa wapo nyuma ya Arsenal kwa tofauti ya alama mbili na mchezo wao ujao utakuwa ni dhidi ya Newcastle United iliyotoka kujeruhiwa na Manchester United kwenye fainali ya Carabao wakati Arsenal ikiumana na Everton.
“Nina hisia kwamba kwenye EPL msimu huu kuna vitu vingi vitatokea. Kila mtu aanaangusha alama, lakini sisi hatutakiwi kuangusha alama nyingi ama kutoangusha kabisa ikiwa tunahitaji kupambana hadi mwisho kwenye vita ya ubingwa,” alisema.
Katika siku za hivi karibuni matajiri ho wa Jiji la Manchester walipitia wakati mgumu kwa kuangusha pointi kwenye mechi dhidi ya Nottingham Forest ambapo walitoka sare sawa na ilivyokuwa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig ambapo walitoka sare kabla ya kushinda kwa mabao 4-1 kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita dhidi ya Bournemouth ugenini.
“Timu yangu inacheza vizuri. Nina furaha na kiwango cha wachezaji wangu namna ambavyo wanapambana. Nilisema baada ya mechi dhidi ya Bournemouth ari na morari kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ni kubwa mno na wachezaji wanapambana sana,” alisema.
Kwa sasa Man City ina alama 55 baada ya kucheza mechi 25 ikishinda 17, sare nne na kufunga nne. Baada ya kucheza na Bristol City jana itacheza na Newcastle United Jumamosi, kisha itavaana na Crystal Palace Machi 11 katika mwendelezo wa EPL.