Manchester United inataka kutumia pesa itakazozipata katika mauzo ya Mason Greenwood katika dirisha hili ili kuipata saini ya mshambuliaji wa Bologna na Uholanzi, Joshua Zirkzee, 23.
Kwa mujibu wa tovuti ya Skysports, mabosi wa Bologna wanahitaji kiasi kisichopungua Euro 40 milioni ili kumuuza Zirkzee. Mkataba wake unamalizika mwaka 2026 na huenda akatua Old Trafford dirisha hili.
EVERTON ipo katika hatua za mwisho kukamilisha dili la kumsajili mshambuliaji wa Marseille na Senegal, Iliman Ndiaye, 24, dirisha hili.
Fundi huyu wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 24, ameivutia Everton baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita na alicheza mechi 46 za michuano yote na kufunga mabao manne.
Everton inataka kumvuta nyota huyu akaongeze nguvu baada ya msimu uliopita kunusurika kushuka daraja.
MSHAMBULIAJI wa Espanyol, Joselu ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Real Madrid yuko kuwa kwenye rada za matajiri wa Qatar, Al Gharafa SC inayohitaji kumsajili dirisha hili. Joselu ambaye mkataba wake na Espanyol unamalizika mwaka 2025, msimu uliopita aliisaidia sana Madrid Ligi ya Mabingwa na alifunga mabao mawili mchezo wa nusu fainali dhidi ya Bayern Munich.
HADI sasa Bayern Munich inadaiwa inaongoza harakati za kuiwania saini ya mshambuliaji wa Barcelona, Marc Guiu, 18, dirisha hili.
Guiu ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango bora msimu uliopita na kuvutia timu nyingi Ulaya na Chelsea pia inahitaji kumsajili.
Mkataba wake unamalizika mwaka 2025. Msimu uliopita amecheza mechi 27 za michuano yote na kufunga mabao tisa.
BORUSSIA Dortmund imetuma barua ya kuulizia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Leeds United, Archie Gray, 18, dirisha hili.
Archie ambaye msimu uliopita alicheza mechi 52, za michuano yote, mwenyewe ameonyesha nia ya kuondoka na kutua Dortmund ili kucheza soka la kishindani zaidi kuliko akiendelea kucheza Leeds ambayo inacheza Ligi daraja la Kwanza.
TOTTENHAM imeingia katika mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wa Lille, Jonathan David, 24, ili kumsajili dirisha hili.
Kitendo cha kuanza mazungumzo na wawakilishi wa staa huyu kinakuwa kimeiingiza Spurs katika vita dhidi ya Chelsea ambayo iliripotiwa kutaka kumsajili kwa muda mrefu na hadi sasa bado wapo katika dili hilo.
LICHA ya tetesi za wiki iliyopita kudai kiungo wa West Ham na Ghana, Mohammed Kudus, 23, yupo katika rada za Al Ittihad ya Saudi Arabia, hadi sasa bado hakuna ofa yoyote iliyowasilishwa mezani kwa West Ham.
Kudus ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango bora msimu uliopita hali iliyovutia timu nyingi kubwa duniani.