Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Goran ageukia ukuta Tabora United

Goran Kapunovic Kitayosce Goran Kopunovic

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya ugeni iliyonayo katika Ligi Kuu Bara, Tabora United imeendelea kuokota pointi na kasi hiyo imempa faraja kubwa kocha wa timu hiyo, Goran Kopunovic aliyekiri kwamba wachezaji wameanza kushika falsafa zake na kwa sasa anageukia mabeki ili kutaka kuzuia kufunga kirahisi inapokuwa uwanjani.

Tabora ni kati ya timu tatu zilizopanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Championship ikiwa ni pamoja na Mashujaa inayocheza pia kwa mara ya kwanza na JKT Tanzania iliyorejea tena katika ligi hiyo na timu hizo zote zinafuatana kwenye msimamo zikitofautiana pointi moja tu baada kila moja kucheza mechi tano.

Mashujaa na Tabora zinalingana pointi na kutofautiana mabao ya kufungwa zikiwa nafasi ya tano na sita mta-walia, huku JKT ikifuata nyuma yao ikikusanya pointi saba na kasi hiyo ya Wafuga Nyuki wa Tabora imemfanya kocha Goran achekelee akiamini kazi yake imeanza kuleta ufanisi mzuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo wa zamani wa Polisi FC ya Rwanda na Simba, alisema licha ya kuimarika kwa timu, lakini ameshtukia makosa rahisi ya mabeki kuruhusu mabao na analifanyia kazi kipindi hiki ligi ikisimama kwa wiki mbili ili watakaporejea wawe imara zaidi kwani anaona falsafa zake zinashikwa.

“Napenda tunavyoendelea kuimarika, sio rahisi hizi mechi lakini unapoona timu inatoka nyuma na kutengene-za ushindi hii ni dalili kwamba wachezaji wameelewa nini tunataka, napenda jinsi tunavyobaki kwenye utulivu wetu wa kucheza soka letu la kuweka mpira chini na kushambulia kwa kasi,” alisema Goran na kuongeza;

“Tumekuwa tunaruhusu mabao rahisi, kuna wakati unaona kama wachezaji wanapoteza umakini kwa wepesi zaidi hili hatutakiwi kuendelea kulitazama tutapambana tuimarishe ukuta, lakini nafurahia namna wachezaji walivyoanza kushika falsafa na timu kucheza vizuri na kupata matokeo mzuri.”

Kocha huyo alisema kwa vile ligi ina michezo mingi mbele yao ni lazima wajipange upya ili wawe imara zaidi kwa kila eneo.

“Changamoto hizi tunahitaji kuzifanyia kazi haraka kabla ya mchezo ujao dhidi ya KMC, niseme ukweli ligi ni ngumu na hatutakiwi kufanya makosa yatakayotupa ugumu kutengeneza ushindi,” alisema Goran ambaye enzi za uchezaji wake alikuwa mshambuliaji kabla ya kugeukia ukocha.

Tabora imeruhusu mabao mawili katika mechi zake mbili ilizoshinda dhidi ya Tanzania Prisons (3-1) kisha ile ya Dodoma waliyoshinda kwa mabao (2-1), lakini ikiwa imeruhusu jumla ya mabao sita kwenye mechi tano za ligi kwa msimu huu na yenyewe kufunga matano.

Katika mechi tano, Tabora imepoteza moja katika mchezo uliokuwa wa kwanza ilipocheza ikiwa na wachezaji wanane dhidi ya Azam na kufungwa mabao 4-0 kabla ya mchezo kuvunjwa dakika ya 15 baada ya wachezaji wawili wa timu hiyo ‘kujivunja’, lakini imetoka suluhu na Singida BS na Coastal Union na kushinda nyingine mbili.

Chanzo: Mwanaspoti