Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Goran, Tabora United kuna kitu kinaendelea

Goran Kopunovic 09 14.jpeg Kocha Mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kauli ya Kocha Mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic kusema anapaswa alaumiwe na kuwajibishwa kwa matokeo mabaya inayopata timu hiyo kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, imeibua sintofahamu juu ya hatima ya kubaki au kung'atuka katika kikosi hicho kinachocheza ligi kwa msimu wa kwanza.

Tabora United haijapata matokeo mazuri kwani imeshinda mechi tatu hadi sasa katika michezo 18 iliyocheza, ikitoka sare tisa na kupoteza sita ikiwa nafasi ya 13 ikikusanya pointi 18.

Goran aliyekabidhiwa kikosi hicho mapema msimu huu hali imeonekana kuwa nźito kwake, huku mashabiki na wadau wa soka mkoani Tabora wakianza kuonyesha dalili za kuikatia tamaa timu hiyo katika hesabu za kubaki Ligi Kuu.

Akizungumza jijini Mbeya mara baada ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Goran amesema matokeo hayo hawezi kumlaumu yeyote isipokuwa yeye ndiye anayestahili kubebeshwa lawama.

Amesema huenda elimu, uwezo, mbinu na juhudi zake zimeshindwa kufanikiwa kwa wachezaji ndio maana matokeo yamekuwa magumu akieleza hajafikiria kung'atuka kutokana na kuwa katika mkataba.

"Kuna mwingine kanitukana 'Mzungu mjinga'. Nimetumia nguvu zote, akili, mbinu, uwezo na uzoefu, lakini sioni mabadiliko yoyote mazuri sasa nifanyeje. Bora nilaumiwe mimi," amesema kocha huyo wa zamani wa Simba na kuongeza:

"Sijafikiria kung'atuka na uamuzi wangu kesho ni kuendelea na programu kikosini japokuwa tayari nimeongea na uongozi kila kitu kujua tatizo nini ila sielewi."

Mserbia huyo ameongeza kwamba anakwenda kukaa tena na wachezaji kuendelea kupambana akikiri kuwa ligi anaiona kuwa ngumu na timu hiyo inahitaji nguvu za ziada ili kuhakikisha inarejea kwenye ubora.

Miezi michache iliyopita zilienea tetesi kwamba kocha huyo alikuwa anaachana na timu hiyo kutokana na kushindwa kutekelezewa baadhi ya mahitaji yake, kabla ya mwenyewe kuweka mambo sawa kuwa ameshamalizana na viongozi na anaendelea na kazi.

Timu hiyo ina mechi nane bila ushindi, kwani ushindi wa mwisho ulikuwa Desemba Mosi, mwaka jana dhidi ya Mtibwa Sugar walioinyoa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Tabora United ilipanda daraja msimu huu sambamba na JKT Tanzania na Mashujaa ya Kigoma iliyopenya kupitia mechi za mchujo (play-off) ikiiishusha Mbeya City.

Chanzo: Mwanaspoti