Kocha msaidizi wa Gor Mahia Sammy ‘Pamzo’ Omollo amemlalamikia wazi wazi mwamuzi aliyechezesha mtanange wa Ligi Kuu nchini Kenya baina yao na Kakamega Homeboyz, kwa kile alichokiita maamuzi mabovu.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika kwa kipigo cha goli 2-1, kocha Omollo alisema inakuwa vigumu kuamini kama hatua ya mashindano makubwa kama ya Ligi kukosa maamuzi bora huku waamuzi wakitoa maamuzi ya upendeleo.
Maneno ya Omollo yanakuja baada ya refarii George Mwai kutoa penati yenye utata katika mechi iliyomalizika kwa ushindi kwa wenyeji Kakamega, penati ambayo kocha anadai kuwa faulo iliyozaa tuta hilo ilikuwa laini na ilikuwa nje ya 18.
“Ilitokea kwenye mechi dhidi ya Mathare United, Posta Rangers, Bandari na imetokea tena kwetu, mechi zote hizo anapewa penati akiwa nyumbani (katika dimba la Bukhungu), tuna mashaka na maamuzi hayo”, alisema kocha Omollo.
Kipigo ambacho Gor Mahia wamekipata kutoka kwa vijana wa Kakamega Homeboyz kinahitimisha safari ya kutopoteza mechi kwao katika mbilinge za Ligi.