Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes azigwaya Azam, Dodoma

C8a739f72f52d83689c641a404a1146f Gomes azigwaya Azam, Dodoma

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Simba, Didier Gomes amezigwaya timu za Dodoma Jiji na Azam akisema mechi dhidi yao zitakuwa ngumu lakini wanatarajia watafi kia malengo waliyojiwekea.

Simba itacheza na Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma kesho kabla ya kucheza na Azam mwishoni mwa wiki hii.

Simba bingwa mtetezi wa Ligi Kuu inatarajiwa kuondoka leo kuelekea makao makuu ya nchi kwa ajili ya mechi hiyo ambako pia imealikwa bungeni na wabunge wanachama wa Simba kwa ajili ya kupeleka kombe la michuano ya Simba Super Cup iliyolitwaa wiki iliyopita.

Michuano hiyo ya Simba Super Cup iliyoandaliwa na klabu hiyo na kushirikisha timu za TP Mazembe ya Congo DR na Al Hilal ya Sudan na Simba yenyewe. Kocha Gomes aliliambia gazeti hili jana kuwa, mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ni muhimu kwao kushinda ingawa anaona hautakuwa rahisi.

“Mechi yetu ya Dodoma na Azam FC zitakuwa ngumu ila lengo letu ni kupambana na kushinda na kufikia lengo lililowekwa la kufanya vizuri kuelekea katika utetezi wa taji,” alisema.

Gomes alisema mechi mbili za kimataifa walizocheza hivi karibuni zimeonesha mwanga kwamba wako vizuri hivyo anatarajia timu itafanya vizuri sio tu kwenye ligi bali hata michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba iliifunga Al Hilal mabao 4-1 kabla ya kutoka suluhu na TP Mazembe ikionesha uwezo na namna ilivyojipanga kupambana kitaifa na kimataifa.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa Gomes tangu achukue mikoba ya kocha Sven Vandenbroeck aliyesitisha mkataba na Simba baada ya kupata ofa nono Morocco.

Wekundu hao wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu na iwapo watashinda viporo vyao viwili dhidi ya Dodoma na Azam FC watakuwa wanaipumulia Yanga karibu kwa tofauti ya pointi tatu.

Yanga inaongoza ikiwa na pointi 44 katika michezo 18 na Simba nafasi ya pili kwa pointi 35 katika michezo 15. Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema baada ya mchezo huo jijini Dodoma Ijumaa watarudi Dar es Salaam kujiandaa na kiporo kingine dhidi ya Azam FC utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkapa.

Wenyeji Dodoma Jiji juzi walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya Fountain Gate na kufungwa bao 1-0 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo na Simba. Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makata alisema mchezo huo umesaidia kuwarudisha wachezaji wake utimamu wa mwili kwani walikaa muda mrefu bila kucheza.

Chanzo: habarileo.co.tz