Zikiwa zimesalia siku sita tu kabla ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes amewaagiza wachezaji wote ambao wapo kwenye majukumu ya timu za Taifa, kuripoti mapema kambini mara tu baada ya kumaliza majukumu hayo, ili kujiandaa na mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa.
Simba inawakosa wachezaji 15 ambao wameitwa katika vikosi vyao vya timu za Taifa kwa ajili ya michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu kombe la Dunia Qatar mwaka 2022, ambapo ratiba ya michezo hiyo kwa michezo ya mzunguko wanne itamalizika leo Jumanne.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu wanatarajiwa kuanzia ugenini nchini Botswana Oktoba 17, mwaka huu mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Gomes amesema: “Kikosi chetu kinaendelea vizuri na maandalizi za mchezo wetu wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, tunajua utakuwa mchezo mgumu hasa kutokana na ubora wa wapinzani wetu, ambao walianzia hatua ya awali ya michuano hiyo na kufuzu kwa ushindi mkubwa.
“Changamoto tuliyonayo ni ile ya baadhi ya nyota wetu muhimu kuwa katika majukumu ya timu zao za taifa, lakini tayari nimewasiliana na Uongozi kwa ajili ya kuhakikisha wachezaji wote ambao wapo katika majukumu ya timu zao za Taifa wanaripoti kambini haraka inavyowezekana, baada ya kumaliza michezo hiyo ili tupate muda wa kujiandaa na mchezo dhidi ya Galaxy.”