Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes: Dawa ya AS Vita inachemka

620a96a755d92b27b769993bf891d06e.jpeg Gomes: Dawa ya AS Vita inachemka

Fri, 26 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema atawashangaza AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo kwani amepata dawa yao.

Simba inacheza na AS Vita katika mchezo wa raundi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Aprili 3, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Gomes alisema amefanikiwa kuwaona katika mechi za hivi karibuni walipocheza na Al Ahly na kutamba amepata dawa ya kuwatuliza katika mchezo.

Gomes alisema ameona tofauti katika mechi yao dhidi ya Al Ahly na hiyo ilimpa somo la kubadilisha mfumo ambao atautumia watakapokutana.

Alisema AS Vita walicheza soka la ya ushindani na walionesha mabadiliko kwa kucheza kimbinu tofauti na walipokutana nao Kinshasa katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi.

“Nimeona wameimarika, nafanyia kazi kuhakikisha AS Vita hawaondoki na pointi katika mchezo ujao. Tunatambua utakuwa mchezo wenye ushindani kwa sababu AS Vita hawakubali kufungwa mara mbili na sisi tunahitaji kutumia uwanja wa nyumbani vizuri,”.

“Huu ni mchezo muhimu kwetu na nina imani wachezaji wangu watapambana ili kupata ushindi kwa ajili ya kujiimarisha na kufuzu hatua ya robo fainali,” alisema Gomes.

Aliongeza atawahimiza wachezaji wake umuhimu wa kushinda mechi hiyo na kukamilisha kazi yao waliyoianza vyema badala ya kusubiri mchezo wa mwisho ambao pia hautakuwa mwepesi kwao.

“Kila mchezaji anajua majukumu ya kufanya uwanjani, nina imani na uwezo wa wachezaji wangu katika kusaka ushindi katika mchezo huo,” alisema. Naye Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema wamejipanga kila idara kuhakikisha wanasonga mbele katika michuano hiyo pamoja na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mangungu alisema wachezaji wote waliobakia hapa nchini wanaendelea na mazoezi na wanajua kiu ya mafanikio ambayo mashabiki na wanachama wa Simba wanatamani kuifikia msimu huu.

“Nimezungumza na kocha wetu, amesema wachezaji waliobaki wanaendelea na mazoezi na kila mmoja ana shauku ya kufanya vizuri katika mchezo huo ambao tunaamini utakuwa na ushindani mkubwa,” alisema Mangungu.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Februari 12, Kinshasa, Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 na mchezo wa mwisho dhidi ya Al Merreikh walishinda mabao 3-0.

Chanzo: www.habarileo.co.tz