Mshambuliaji wa AC Milan, Olivier Giroud alilazimika kwenda kusimama langoni katika ushindi wa bao 1-0 wa Serie A waliopata dhidi ya Genoa.
Na mashabiki walimsifu mshambuliaji huyo wakidai kuwa ni bora kuliko kipa wa Manchester United, Andre Onana baada ya kuokoa mpira usiingie langoni kwao.
Giroud, 37, bado anacheza katika kiwango cha juu baada ya kukipiga Arsenal na Chelsea. Fowadi huyo yuko katika msimu wake wa tatu akiwa na Milan na tayari amefunga mabao manne katika mechi sita.
Fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliibuka kuwa shujaa wikiendi iliyopita wakati wababe hao wa Italia waliposafiri katika jiji la Genoa kwa ajili ya pambano kali la Serie A.
Baada ya kupambana katika mechi hiyo Milan ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 87 lililofungwa na winga wa zamani wa Chelsea, Christian Pulisic.
Lakini maafa yalitokea katika dakika ya nane ya muda wa majeruhi ambapo kipa Mike Maignan alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kutoka nje ya eneo la hatari na kumwangusha fowadi wa Genoa.
Hapo ndipo uamuzi ulipofanyika kuwa Giroud akasimame langoni kuokoa jahazi kwani wapo pungufu huku mpira ukielekea ukingoni kumalizika.
Mashabiki waliibuka katika mtandao ya kijamii wakimsifu baada ya kuokoa mpira wa hatari kabla kipenga cha mwamuzi kupulizwa.
Shabiki mmoja aliandika: "Giroud ni zaidi ya kipa wa Manchester United, Andre Onana. "Mwingine akaandika: "Giroud hakuruhusu bao na ameongeza rekodi nyingine kwa ajili yake."