Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gilbert Kaze: Kitasa cha Simba kilichowaumiza Yanga

Gilbert Kaze0003 Gilbert Kaze

Wed, 30 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukiondoa mchezo wa Yanga kuwahi kupoteza kwa mabao 5-0 dhidi ya Simba kama kuna mchezo mwingine uliowahi kuwaumiza Wanajangwani basi ni ile sare ya mabao 3-3 dhidi ya watani wao hao.

Kwenye matokeo hayo, Yanga ambayo ilitangulia kuongoza kwa mabao 3-0 hadi mapumziko, Simba walirudi na nguvu ya ajabu kipindi cha pili na kuyarudisha yote na aliyefunga bao la tatu la wekundu hao alikuwa beki Mrundi Gilbert Kaze.

Kaze yuko hapa nchini akiwa mmoja wa wachezaji wa kikosi cha ASAS ya Djibout iliyocheza na Yanga kwenye mchezo wa awali wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalum

MAISHA YA DJIBOUT YAKOJE?

“Maisha ya Djibout yako poa, kila kitu kinakwenda vizuri, sawa huwezi kulinganisha na hapa Tanzania kwa kuwa ile ni nchi ambayo inaendelea kukua na kubadilika taratibu lakini tunamshukuru Mungu kila kitu kinakwenda kama ambavyo tulitarajia,” anaeleza Kaze akianza kuelezea maisha ya soka nchini Djibouti anakocheza sasa.

BAADA YA KUONDOKA SIMBA

“Nakumbuka hapa nilicheza nikiwa Simba kwa msimu wa 2013/14, baada ya kuondoka hapa Tanzania nilirudi nyumbani nikacheza ligi ya nyumbani kwa misimu kama mitatu nikianza Vital’O kisha Lydia Ludic Akademi ya Burundi pia niliitumikia kwa misimu miwili baadaye ndio nikaona ni wakati wa kurudi kucheza nje nikapata nafasi hii ya kuja Djibouti ambako niko mpaka sasa, anaeleza Kaze.

“Nikiwa Djibouti nilianzia timu ya Chuo Kikuu cha Djibuti nilicheza pale kwa miaka kadhaa na baadaye nikahamia hapa ASAS ambako niko mpaka sasa kwa miaka miwili.

ILIKUWAJE AKAONDOKA SIMBA

“Kuondoka kwangu Simba kulitokana na kukutana na wakati mgumu kwasasabu Simba nilisaini miaka miwili lakini nilipocheza nusu msimu kwenye ule mwaka wa kwanza nikapata majeraha kwa hiyo ile nusu ya msimu wa kwanza nzima nilikuwa najiuguza, nikiwa najiuguza na goti klabu ikaniambia wataniacha na kweli waliniacha nikarudi nyumbani Burundi kuna makubaliano tulikubaliana ingawa kuna sehemu hawakumaliza nawadai dola 6000 Simba mpaka leo hawajanipa, niliwahi kuwasiliana na shirikisho la hapa hawakunipa majibu juu ya madai yangu.

TAMBWE ALIMVUTA SIMBA

“Unajua kuja kwangu Simba ni Tambwe (Amissi) ndiye aliyenipendekeza kwa viongozi wa Simba, nakumbuka yeye (Tambwe) ndiyo alitangulia kuja Simba, alipofika hapa akaambiwa pia timu inatafuta beki wa kati ndio hapo akawaambia kuna beki anamjua na kweli Simba walinitafuta nikaja.

“Nilipofika ni kweli walinipokea vizuri na nilianza kazi vizuri licha ya changamoto za kiuchumi lakini tulionyesha juhudi kubwa za kuipigania jezi ya Simba mpaka pale nilipopata majeraha, kitu ambacho kiliniuma sikuwahi kuwa na matatizo ya goti kabla ya kupata nikiwa hapa.

CHANGAMOTO SIMBA WAKATI HUO

“Changamoto ya Simba wakati huo timu ilikuwa inaundwa na wachezaji wengi waliotoka timu B ya vijana, ilikuwa kama tunaanza kusuka timu mpya ambayo wachezaji wengi walikuwa vijana na sisi wenye uzoefu kidogo, jingine kubwa wakati huo Yanga walikuwa vizuri na hizi kama unavyojua hizi timu kubwa zina maisha ya kuangaliana.

“Yanga walikuwa na kikosi chenye wachezaji waliokomaa vuzuri na viwango vikubwa wa hapa Tanzania na wale wa kigeni nisiseme uongo timu yao ilikuwa kabambe ukilinganisha na huku kwetu tulikuwa na kina Mkude (Jonas), Chanongo (Haruna) Sheva (Miraji Athuman) kwahiyo huku kwetu tulikuwa tunatakiwa kupambana sana kupata matokeo.

“Makocha pia walikuwa wa hapa Tanzania tulikuwa na kocha Julio (Jamhuri Kihwelo) na Mzee Kibaden (Abdallah) pia kifedha hatukuwa tunaonekana kama Simba ilikuwa na maisha mazuri ukilinganisha na Simba ya sasa kwahiyo changamoto zilikuwa nyingi, nakumbuka bonasi ya kushinda mechi tuliambiwa tunapata asilimia za mapato kwahiyo ilitufanya wachezaji kujituma sana ili tushinde tupate bonasi.

MECHI YA 3-3 DHIDI YA YANGA

“Niseme ukweli tulikuwa na hali ambayo haikuwa nzuri wakati tunaelekea kwenye ile mechi, presha ilikuwa kubwa sana kwetu kabla na hata tulipokuwa tunaingia kwenye ule mchezo, nadhani pia ilichangiwa asilimia kubwa wachezaji wengi walikuwa vijana na mechi ile ilikuwa ya kwanza kwao ya watani, mechi ilipoanza tu kile kipindi cha kwanza tulipoteana vibaya na Yanga wakapata mabao yale matatu.

JULIO ALIKUWA ANALIA

“Tulipokwenda mapumziko, baadhi ya viongozi pia walikuja vyumbani kutuuliza nini kimetukumba, nakumbuka maneno ya kocha Kibadeni alituambia tujaribu kipindi cha pili tusifungwe mabao mengi, hakutuambia twende tukarudishe mabao wala kutupa mbinu za tufanye kipi ili turudishe yale mabao alituambia hivyo tu kwamba tusiende kuruhusu mabao mengi, twende tukazuie wakati huo kocha Julio alikuwa analia tu alidhani tungepigwa tano, sita au saba.

“Sisi kama wachezaji nakumbuka Amri Kiemba alituambia tutulie tupunguze presha tunaweza kufanya jambo hata kupunguza mabao hata kupata moja na tuliporudi kweli tukapata bao moja, tukaongeza presha tukapata lingine Yanga nao wakaanza kuingia presha baadaye nikafunga bao la tatu hali ikabadilika uwanja mzima.

“Yanga wakaonekana kuchanganyikiwa kabisa na mwisho mchezo tukautawala sisi ambao tulionekana tutafungwa nyingi ile mechi ilipoisha Simba tulikuwa kama tumeshinda, viongozi walifurahi na mashabiki wetu walipagawa, ilikuwa mechi ambayo ni vigumu kusahaulika.

“Furaha ya viongozi kwa kufanikisha tu mabao yale kurudi walituongezea fedha kwenye kile kiasi cha awali ambacho walituahidi kabla ya mechi, unajua ni ukweli kwamba tulidhani tungepoteza ule mchezo kutokana na ubora wa Yanga, tulidhani tungepata bao moja au mawili kupunguza makali ya kipigo lakini mwisho yakarudi yote hakuna aliyetegemea yangerudi hata mashabiki tuliporudi kipindi cha pili tuliona wamepungua majukwaani.

ANAFUATILIA SOKA LA BONGO

“Nikiwa Djibouti pia huwa naangalia mechi za ligi ya hapa Tanzania tena sana tu, huwa tunafuatilia kupitia mtandao wa Azam lakini mara nyingi huwa nafuatilia hizi klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam au kama ni timu ndogo basi zile zenye wachezaji wa kwetu kutoka Burundi.

LIGI KUU BARA IMEPIGA HATUA

“Kiukweli ligi ya hapa inapiga hatua sana unaweza usione kwa haraka ukiwa hapa ndani lakini sisi tuliopo nje tunaona hatua kubwa tofauti ya wakati mimi nacheza hapa na sasa ni kubwa mno ushindani ni mkubwa, miundombinu pia inaongezeka kwa ubora, watu wa hapa pia wanainogesha kwa kuwa wanapenda sana mpira.

“Hata kwa klabu Kimataifa nako hatua ni kubwa ukiangalia Simba na Yanga sasa hivi zinafika mbali kuzidi hata hatua ya makundi, haya ni mafanikio makubwa ambayo mataifa mengine yanatamani, ushindani huu unawavutia wachezaji wengi wakubwa kutoka mataifa mbalimbali.

“Uwekezaji pia usisahau hapa wadhamini wanaweka fedha za kutosha, timu zina udhamini binafsi, pia hii inafanya kila timu ijipange kufanya vizuri hapo ushindani unaongezeka.

UJIO WA WARUNDI TANZANIA

Kuna makocha wengi na wachezaji wote wa kutoka Burundi wakija kwa wingi na kuondoka hapa Tanzania wakiacha rekodi mbalimbali Kaze anaeleza wapi raia wenzake walipofanikiwa.

“Nafikiri inatokana na uwepo wa vipaji vingi Burundi, kwa wachezaji unajua kule kwetu tumewekeza sana nguvu kuzalisha wachezaji wakianzia utotoni, hii inafanya ubora wao kuwa mkubwa wakienda maeneo mbalimbali, pia wanakuwa ni wavumilivu wa hali zozote.

“Kule Burundi kuanzia tukiwa wadogo tunafundishwa sana ufundi wa mpira ni kama vile Hispania, ile kijana anakuwa nayo mpaka anakomaa ndio maana huwa tunakuwa na wachezaji wengi wanaoweza kucheza falsafa ya kuuchezea mpira tofauti na hapa unaona watu wengi wanatumia sana fiziki.

“Kwenye makocha nako naweza kusema inatokana na hapa Tanzania timu inapotafuta kocha inaangalia wapi tutapata kocha bora anayejua na mwenye rekodi mbalimbali nafikiri ni hivyo tu.

LIGI YA DJIBOUT

“Ukweli ni kwamba ligi ya Djibuti iko chini huwezi kuilinganisha na hii ya hapa Tanzania lakini kadiri ya muda unavyokwenda inakua taratibu kwa kuwa kwasasa wameanza kuweka nguvu ya uwekezaji kwenye soka, timu zao zimeanza kuchukua wachezaji wa kigeni ingawa sio wenye viwango vikubwa kama hapa Tanzania au Uganda lakini wapo.

“Unaona timu kama Atla Solar kwasasa ndio inachukua wachezaji ghali kama tulivyoona hivi karibuni ilimleta Alex Song na Kalou (Solomon) walikuwa wanalipwa mpaka dola elfu kumi kwa mwezi, shida kubwa ya wachezaji wa Djibouti wanajua mpira lakini hawapendi kuucheza hatujui shida iko wapi, unaweza kukuta mchezaji wa kule anakuja mara mbili mazoezini kwa wiki ndio maana unaona timu yao ya taifa iko chini labda klabu ndio utakuta kuna hatua kidogo zinapigwa.

SIRI KUCHEZA MUDA MREFU

Rekodi zinaonyesha Kaze alizaliwa miaka 38 iliyopita na mpaka sasa bado anacheza soka la ushindani hapa anaeleza siri ya ya kudumu kwake kucheza kwa muda mrefu.

“Naweza kusema ni nidhamu kiujumla wake, mimi mwili wangu haujawahi kugusa kilevi cha aina yoyote kuanzia kinywaji mpaka sigara lakini ukiacha hivyo nikitoka uwanjani siendi klabu wala sehemu yoyote ya starehe, wakati nimefika Simba nilioa kwahiyo wakati wa mapumziko basi ni wakati wa familia na muda mwingine napenda kutumia kumuomba Mungu hayo ndio maisha yangu ya kila siku.”

BADO ANAKIPIGA, AUTAKA UKOCHA

“Mimi kustaafu kucheza soka bado kidogo, najiona bado mwili una nguvu lakini kuhusu maisha yangu ya baadaye nafikiria kuwa kocha wa soka, tayari kuna mambo ambayo shirikisho la kwetu wamefanya na mimi ili nianze hiyo kazi.”

SOKA BONGO LIMEMPA KIPI

“Namshukuru Mungu fedha ambayo niliipata hapa nilinunua kiwanja na nimejenga nyumba yangu ya familia, ambayo ndiyo naitumia na watoto na mke wangu kule Burundi.

SAIDO WA SIMBA, YANGA

“Soka la hapa Tanzania linakua sana unajua maisha ya ushindani yanaanzia kwa viongozi unaona Yanga, Hersi Said (Rais) anaweka fedha hii na huku MO Dewji naye anasema sikubali ataongeza hiki kule Azam nako kiongozi wao Bakhresa ataweka chake huu ushindani unakwenda mpaka kwa wachezaji lakini kikubwa presha ya mashabiki nayo inachangia sana maendeleo hasa kwa klabu za Simba na Yanga.

Hii ipo hasi kwetu Burundi nako mashabiki wa Simba na Yanga wako na waliongezeka zaidi alipohamia Saido Ntibazonkiza pale Yanga Warundi wengi walikuwa ni mashabiki wa Yanga hata mimi nilikuwa shabiki wa Yanga kwa muda unajua Saido ni mchezaji mkubwa wa mfano kule kwetu lakini alipohamia Simba mashabiki wengi wamehama na kuja Simba.

Chanzo: Mwanaspoti