Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gia ya baiskeli yamkwamisha shabiki Yanga kuiona CR Belouizdad

Shabiki Pc Yanga Gia ya baiskeli yamkwamisha shabiki Yanga kuiona CR Belouizdad

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shabiki maarufu wa Yanga, Iddi Mkhuu (71), aliyekuwa akisafiri kwa baiskeli kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam kutazama mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad amekwama mkoani Kilimanjaro baada ya baiskeli yake kufeli gia.

Shabiki huyo maarufu kwa jina la 'Kitambi Noma' amekuwa maarufu akitumia usafiri wa baiskeli kusafiri safari ndefu kwenda kuiona timu ya Wananchi kila inapocheza mechi kubwa.

Yanga inajiandaa na mchezo wa kundi D wa raundi ya tano ya  hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam wikiendi hii ambapo itacheza na CR Belouizdad ya Algeria.

Akizungumza na Mwanaspoti, shabiki huyo amesema amekwama kuendelea na safari baada ya kupata hitilafu ya baiskeli anayoitumia kusafiria kufeli gia akiwa mkoani Kilimanjaro ambapo ameuomba uongozi wa timu hiyo kumnunulia nyingine.

"Baada ya kufika Mkoa wa Kilimanjaro nilipata break down kidogo baiskeli ikawa imefeli gia kukawa hakuna uwezekano wa kuiendesha ikabidi niiweke pembeni nitafute msaada mwingine ili niweze kufika," amesema Mkhuu.

Amesema mbali na changamoto ya kuharibikiwa baiskeli, pia amezitaja nyingine zikiwemo za kukumbana na  wanyama wakali porini, kukosa sapoti na fedha za kujikimu pamoja na maneno ya  kukatishwa tamaa yanayotolewa na baadhi ya mashabiki.

Akielezea sapoti aliyowahi kupata kutoka Yanga, Mkhuu amekiri uongozi umewahi kumpatia Sh70,000 pamoja na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Fiston Mayele aliyempa Sh50,000 huku akiahidiwa kufanyiwa mambo mengi ambayo mpaka sasa anadai hayajatekelezwa.

Shabiki huyo amefurahi kwa wema aliyowahi kutendewa na wanananchi wa Kilimanjaro wakati akisubiri msaada akihofia  kukosa kuuona mchezo wa Yanga na Belouizdad ambao ni muhimu  kwa timu yake. 

Kitambo Noma ambaye anadai ni mstaafu serikalini, amesema ameomba pia timu hiyo imwezeshe kupata baiskeli mpya kwani anayotumia ni ya zamani tangu 1982.

Baadhi ya mashabiki mkoani Kilimanjaro wamemtaka shabiki huyo kuitumikia Yanga pasipo kutegemea msaada wala malipo kutoka kwa viongozi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: