Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ghafla stori ya Novatus imebadilika Shakhtar

Novatus Dismas 40 Novatus Dismas

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mambo yamebadilika kwa kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Novatus Dismas huko Ulaya ambako anacheza soka la kulipwa akiwa na FC Shakhtar Donetsk, tofauti na awali ambapo alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa sasa amejikuta akisugua benchi kiasi cha wadau mbalimbali kuhoji nini kimemkuta.

Novatus ambaye alijiunga na Shakhtar kwa mkopo akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji, alianza vizuri maisha yake ya soka huko Ukraine kwa kupata nafasi ya kucheza michezo minne mfululizo mara tu baada ya kukamilisha usajili wake, ikiwemo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto.

Ndani ya michezo hiyo ambayo alitumika kama beki wa kushoto, Shakhtar ilishinda mara moja kwenye kombe la ligi dhidi ya Veres Rivne kwa mabao 3-0, sare pia moja dhidi ya Rukh Lviv kwa bao 1-1, walipoteza mara mbili dhidi ya FC Porto kwa mabao 3-0 na Vorskla Poltava kwa mabao 2-1.

Tangu hapo mambo yakaanza kumwendea kombo kwa kukaa benchi katika michezo minane mfululizo ya mashindano yote kabla ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) ambazo zilifanyika Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka huu, 2024.

Hata baada ya kumalizika kwa fainali hizo ambazo Tanzania ilishiriki kwa mara ya tatu, bado mambo yaliendelea kuwa vile vile kwa mchezaji huyo licha ya kwamba alipata nafasi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Velez Mostar na alicheza kwa dakika 90 ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Europa League.

Shakhtar ilijikuta ikiangukia kwenye michuano hiyo baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi H la Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kuwa sehemu ya maandalizi ya mchezo huo ambao ulikuwa dhidi ya Marseille hakuwa hata sehemu ya wachezaji wa akiba kwenye mchezo wa kwanza ambao walitoka sare ya mabao 2-2.

Waliposafiri na kwenda Ufaransa kwa ajili ya mchezo wa marudiano, kocha wa kikosi hicho, Marino Pusic alisafiri na mchezaji huyo lakini aliishia kukaa benchi wakati

Shakhtar ikifungashiwa virago kwenye michuano hiyo baada ya kutandikwa mabao 3-1.

MCHAWI WA NOVATUS

Nani mchawi wa Novatus? Irakli Azarovi ndiye chaguo la kwanza kwa sasa upande wa beki ya kushoto kwenye kikosi cha Pusic, nyota huyo wa kimataifa wa Georgia amepata shavu la kucheza michezo 20 kwenye mashindano yote.

Beki huyo ametoa asisti mbili, ametumikia katika dakika 1,479 huku Novatus akicheza kwa dakika 347 katika mechi sita tu.

Hivyo Novatus ana kibarua kizito cha kufanya kuhakikisha anarejea kwenye kikosi cha kwanza cha Pusic ambaye amekuwa akipendelea kucheza na mabeki wa nne nyuma na hubadika muda mwingine na kucheza na watatu.

Wakati akiwa Ubelgiji, Novatus alikuwa na uwezo wa kutumika kama sehemu ya mabeki watatu wa kati lakini akicheza kushoto na alipohitaji kucheza pembeni zaidi kama beki wa kisasa mwenye jukumu la kupanda na kushuka aliwajibika vilivyo na ndio maana Shakhtar ilivutiwa naye.

Lakini pia Novatus anaweza kutumika kama kiungo mkabaji hiyo ndiyo nafasi ambayo Watanzania wamemshuhudia akicheza tangu akiwa Biashara United ya Mara kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara na hata upande wa timu ya taifa.

NJIA YA BALE

Novatus anaweza kuamua kupita njia ambayo aliitumia nyota wa zamani wa Tottenham, Gareth Bale ambaye wakati akiwa hana nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, alijitoa sana kwenye uwanja wa mazoezi na kusubiri siku ambayo kocha wake, Harry Redknapp atampa nafasi.

Bale ambaye alianza kucheza kama beki wa kushoto wakati ambao Tottenham ikosa huduma ya Benoit Assou-Ekotto, ilibidi apewe nafasi na ndio ukawa mwanzo wake wa kucheza mfululizo kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo hata baada ya mwenye namba kurudi Redknapp alitafuta namna ya kumtumia mchezaji huyo.

Hivyo Novatus anaweza kuwa na hesabu kama za Bale ambaye alitundika daruga akiwa na Real Madrid, umri wake unaruhusu yapo mazingira ambayo yanaweza kumfanya kocha wake huko Shakhtar kumtumia na hapo ndipo anaweza kumuonyesha kwamba alifanya makosa kutompa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho.

Kati ya mechi ambazo zilimpa ujiko Bale ni pamoja na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2010 kati ya Tottenham na Inter Milan alimfanya Maicon kulala na viatu.

WADAU UKRAINE

Ivanna na Daryna Michael ni mtu wa mdogo wake huko Ukraine ambako anacheza soka la kulipwa Novatus, wanaamini mchezaji huyo kuwa ana uwezo wa kubadili hiki ambacho kinaendelea na kufanya makubwa akiwa na Shakhtar.

Daryna ambaye ni injinia, amesema, “Sijawahi kupata nafasi ya kuongea naye lakini ni mchezaji mzuri, ipo mifano mingi ya wachezaji ambao hawakuanza vizuri hapa Shakhtar lakini kwa sasa wanafanya vizuri, anahitaji muda Nova.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live