Ghafla Manchester United imeibuka na kutajwa kama moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kumsajili straika wa Napoli, Victor Osimhen kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, imeelezwa.
Staa huyo wa Napoli, Osimhen, 25, anajiandaa kwa ajili ya kuwa sokoni wakati dirisha litakapofunguliwa, huku mkataba wake ukielezwa kuwa na kipengele kinachohitaji ilipwe Pauni 94 milioni kwa timu itakayohitaji kumsajili.
Man United inajiandaa na mipango ya kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha lijalo hasa baada ya ujio wa tajiri kubwa, bilionea Sir Jim Ratcliffe.
Kwa mujibu wa Independent, Osimhen anatazamwa kama mpango sahihi wa usajili wa mabosi wa Man United kutokana na umri wake huku wakiamini ataweza kwenda kuzoea mazingira kwa haraka.
Endapo kama Man United itafanikiwa kumnasa Mnigeria huyo na kumleta Old Trafford, atawapa machaguo tofauti na Rasmus Hojlund kwenye fowadi ya timu hiyo, eneo ambalo lina tatizo.
Anthony Martial anajiandaa kuondoka bure mwisho wa msimu, wakati Marcus Rashford anacheza vizuri zaidi akiwa kwenye upande wa kushoto. Kuhusu Osimhen mkataba wake umebakiza miaka miwili Napoli.
Wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England, Chelsea na Arsenal nazo zinahitaji huduma ya straika huyo wa zamani wa Lille, huku gwiji wa The Blues, John Obi Mikel akidai staa huyo anakwenda Stamford Bridge.
Paris Saint-Germain nayo inamtazama mchezaji huyo kama mbadala muhimu wa kwenda kuchukua buti za Kylian Mbappe, ambaye anaripotiwa kuwa na mpango wa kutimkia Real Madrid mwishoni mwa msimu.
Osimhen tangu alipojiunga na Napoli amefunga mabao 72 katika mechi 123 na kuisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Serie A msimu uliopita. Msimu huu ameshafunga mabao 11 katika mechi 16 za ligi.
MAVITU YA OSIMHEN 2023-24
-Amecheza: Mechi 16
-Ametengeneza: Nafasi 11
-Amefunga: Mabao 11
-Ametoa: Asisti 3
-Amelenga goli: Mashuti 20
-Amepiga: Pasi 147