Timu ya Gets Program ya Dodoma imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kwa Wanawake (WRCL) baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwanga City ya Kigoma.
Mchezo huo wa fainali umepigwa leo kuanzia saa 9:30 alasiri katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ukihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walace Karia na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla.
Mtanange huo umekuwa mgumu kwa timu zote mbili kutokana na ubora wa vikosi vyao kwani zimefika hatua hiyo bila kupoteza mchezo, bao pekee kwenye mchezo huo limefungwa na Eva Sady dakika 48.
Fainali hiyo inetanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu kati ya Mpaju Queens ya Mbeya na Sayari Women ya Dar es Salaam, ambapo Mpaju imeshinda bao 1-0 likifungwa na Martha Meja.
Timu hizo nne, Gets Program, Mwanga City Queens, Mpaju Queens na Sayari Women zimepanda kucheza Daraja la Kwanza Tanzania Bara (WFDL) msimu ujao (2023/2024).
Mbali na ubingwa na kukabidhiwa kombe na medali, Gets Program imezoa tuzo ya mfungaji bora, Irine Chitanda aliyefunga mabao 13 na mchezaji bora wa mashindano (MVP), Beatrice Charles.
Kipa wa Mwanga City, Habi Faida ameibuka kuwa kipa bora wa mashindano na Chipuputa Queens ya Mtwara ikiibuka kuwa timu yenye nidhamu.
Kocha wa Gets Program, Aristides Given, amesema siri ya mafanikio hayo ni wachezaji wake kutafsiri vyema maelekezo yake uwanjani, huku Kocha wa Mwanga City, Kashinde Mangapi, akiwapongeza wachezaji kwa kufikia hatua hiyo na kukiri kuwa wamekabiliana na timu ngumu ambayo imesheheni wachezaji wenye uzoefu.
Ligi hiyo ambayo ni msimu wake wa pili ilianza Julai 17, mwaka huu na kuhitimishwa leo Julai 27, 2023 ikishirikisha timu 19 kutoka mikoa 18 ya Tanzania Bara huku michezo 44 ikipigwa katika Uwanja wa Nyamagana na CCM Kirumba, Mwanza.