Baada ya kuwa nje kwa miezi mitano tangu alipofungashiwa virago vyake ndani ya Aston Villa, Steven Gerrard anatarajia kurejea kwenye kazi ya ufundishaji na safari hii anatarajia kuwa kocha mpya wa Trabzonspor ya Uturuki.
Gerrard anatarajiwa kuwa kocha wa timu hiyo baada ya juzi Jumamosi kwenda nchini humo kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho kabla ya kukabidhiwa rasmi mikoba ya kuanza kuifundisha timu hiyo.
Kiungo huyo wa zamani wa Liverpool amekaa nje kwa miezi mitano kwenye kazi hiyo ya ukocha tangu mara ya mwisho Oktoba mwaka jana alipokuwa akiifundisha Aston Villa ambayo alifukuzwa kutokana na matokeo mabaya, akishinda mechi mbili pekee kwenye 11.
Baada ya kutua Uturuki, Gerrard alitarajia kula chakula cha usiku na makamu wa rais wa timu hiyo, Ertugrul Dogan na kujadiliana zaidi kuhusiana na dili hilo.
Muingereza huyo anatarajiwa kuchukua mikoba ya kocha Abdullah Avcı ambaye alifukuzwa kwenye nafasi hiyo baada ya kufungwa wiki iliyopita na vibonde, Umraniyespor kwa mabao 2-1.