Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kupitia EFM Radio, Geoff Lea amesema Yanga SC hawana kikosi kipana ndiyo maana baada ya kufanya rotation ya wachezaji saba walifungwa bao 2-1 na Ihefu FC.
"Unajua tunatofautiana kuhusu hii dhana ya kufanya mabadiliko ya kikosi. Mtu anayewajibika kwenye uwezo wa wachezaji ni kocha."
"Mabadiliko ya kikosi hufanyika kwa lengo la kuwapumzisha wachezaji (ambao wanatumika sana), lakini mara nyingi utakuta ule uwiano wa dakika hauwapi wachezaji wengine nafasi ya kuwafikia wenzao na matokeo yake kuna tofauti kubwa sana ya wachezaji wanaoanza kwenye kikosi cha kwanza na ambao huwa hawaanzi.
"Kama Kennedy Juma amekuwa Simba kwa muda mrefu lakini amecheza dakika chache sana.
"Sidhani kama kwa sasa hivi tunaweza kusema Yanga wana kikosi kipana, hasa kwa kuzingatia muitikio hasi wa mashabiki wa Yanga kwa kocha wao kwa aina mabadiliko aliyoyafanya.
"Kwa kocha kila mchezaji ni muhimu lakini kwa Presha anazozipata (Gamondi) na kwa matokeo yale ya Ihefu, pengine hatutoona tena kocha akifanya mabadiliko ya kikosi, maana akipoteza tena pointi matokeo yake anaenda kupoteza ubingwa. Kwa sasa ilivyo, Yanga hawana kikosi kipana,” amezungumza Mchambuzi wa soka Geoff Lea kupitia EFM Radio.