Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita yatakata Nankumbu, Mpole kama Mayele

Geita Win Kageraa Wachezaji wa Geita Gold wakishangilia goli la Mpole

Sat, 7 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kuinyuka Azam FC leo Kagera Sugar imekwaa kisiki ugenini na kuendeleza uteja mbele ya Geita Gold msimu huu kwenye mechi za Ligi Kuu ikipoteza michezo yote miwili.

Kagera imepoteza mchezo wa pili wa ligi msimu huu kwa majirani zao, Geita Gold baada ya kuchapwa bao 1-0 kwenye mtanange uliopigwa leo uwanja wa Nyankumbu mjini Geita ambapo wenyeji wamepaa hadi nafasi ya tatu kutoka ya saba wakifikisha pointi 31 huku Kagera wakisalia kwenye nafasi ya sita na alama 29.

Msimu huu timu hizo zimekutana mara nne, mara mbili zikiwa ni mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu ambapo Geita ilishinda moja na kutoka sare huku zikikutana mara mbili kwenye ligi ambapo wachimba Dhahabu wameshinda zote.

Bao pekee la ushindi la wachimba Dhahabu hao limepachikwa dakika za mapema za mchezo huo na George Mpole mnamo dakika ya tatu kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi ya kichwa kutoka kwa Chilo Mkama uliotokana na kona iliyochongwa na Edmund John.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuifanya Geita Gold kwenda mapunlmziko ikiongoza kwa bao 1-0 huku wakiwadhibiti Kagera ambao walishindwa kupiga shuti lililolenga goli wala kona hata moja wakati Geita ikipiga kona tatu ndani ya dakika hizo.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya kiufundi kujaribu kuongeza mabao na kusaka ushindi ambapo Kagera Sugar waliwatoa Yusuph Dunia, Meshack Abraham na Jordan John nafasi zao zikichukuliwa na Hassan Mwaterema, Amissi Kiiza na Abdallah Seseme huku Geita wakitoka Yusuph Kagoma, Edmund John, Dany Lyanga na Geofrey Manyasi na kuingia Juma Mahadhi, Paul Luchagula na Offen Chikola lakini dakika 90 zilimalizika kwa ushindi huo wa 1-0.

Baada ya kufunga bao hilo leo rasmi George Mpole anamfikia nyota wa Yanga, Fiston Mayele wakilingana mabao 12 kwenye ligi na kuzidi kuongeza ushindani kwenye vita ya ufungaji kuwania kiatu cha dhahabu huku Reliant Lusajo wa Namumgo akiwafuatia kwa karibu na mabao yake 10.

Mnamo dakika ya 15 nusura George Mpole aiandikie bao la pili timu yake baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Kagera kufuatia kipa wa timu hiyo, Chalamanda kuutema mpira lakini shuti la Mpole likapaa kidogo juu ya lango.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live