Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita yaahidi kupiga kwenye mshono

Morocco X PRESS Kocha Mkuu wa Geita Gold, Hemed Suleman 'Morocco'

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema mchezo wa kesho dhidi ya Yanga utakuwa mgumu, lakini tayari wamefanya tathmini na kujua sehemu ya kuikamatia na kuimaliza.

Wachimba Dhahabu hao wa mjini Geita, kesho watakuwa wenyeji wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Morocco amesema timu hizo zinakutana baada ya kupoteza michezo iliyopita hivyo kila moja itapambana kupata ushindi, lakini yeye ameshamaliza hesabu na vijana wake kwani ana imani kubwa wanakwenda kuvunja mwiko wa kutopata ushindi dhidi ya Yanga.

Amesema kwa siku tatu ambazo wamekuwa jijini Mwanza wakijifua, wamefanya maandalizi mazuri na wachezaji wamefuata maelekezo ambayo yatawapa ushindi kwani kikosi kina hali nzuri na kiko tayari kwa mchezo.

"Sote tumepoteza mechi zilizopita tunajua mechi itakuwa ngumu, lakini nimejaribu kuwatengeneza wachezaji wangu kisaikolojia. Kwa hiyo sisi kama Geita tumesimama vizuri, naamini tutapata ushindi," amesema Morocco.

"Yanga ni timu nzuri imekuwa na mtirirko mzuri wa kiwango na matokeo na mchezo utakuwa wa mbinu. Kwa hiyo mwenye mbinu nzuri ndiye atakayeshinda. Najiamini kwa ajili ya wachezaji wangu jinsi tulivyojiandaa tumeangalia udhaifu wa Yanga naamini tuna nafasi ya kufanya vizuri.

"Tunawaheshimu Yanga, tunajua ni timu nzuri inaweza kupata matokeo popote. Tumefanya mazoezi, mimi naamini itakuwa mechi ya aina yake, nzuri na tutapata matokeo kuondoa rekodi za nyuma za kufungwa kila wakati na Yanga."

Mchezaji wa timu hiyo, Samwel Onditi amesema hawana hofu kuhusu Yanga kwani wamejiandaa vizuri kupata ushindi kutokana na maelekezo ya makocha ambao wamefanyia kazi upungufu walionao Yanga na ubora, hivyo watakwenda kuyafanyia kazi ili wawe na mchezo mzuri mbele ya mashabiki.

"Wachezaji tumezungumza mambo mengi na tumejipanga. Ni mchezo kama mingine, tunafahamu (Yanga) wana wachezaji wazuri, lakini hatuna hofu wala shaka kwa mchezo wa kesho. Kikubwa ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi," amesema Onditi.

Chanzo: Mwanaspoti