Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita wapanga kuvuruga rekodi ya Yanga

Geita Broke Record Geita wapanga kuvuruga rekodi ya Yanga

Thu, 27 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Joto la mchezo wa Ligi Kuu kati ya Geita Gold na Yanga limezidi kupanda huku uongozi wa Wachimba Dhahabu ukichimba mkwara kuwa tambo za Yanga kutopoteza mchezo wa ligi zitakoma Jumamosi.

Mchezo huo utapigwa keshokutwa Jumamosi saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza viingilio vikiwa Sh 20,000 (jukwaa kuu), Sh 10,000 (jukwaa la kawaida) na sh 5,000 mzunguko huku Yanga ikiwa na kumbukumbu na kuifunga Geita Gold katika uwanja huo msimu uliopita.

Akizungumza leo Oktoba 27, 2022 katika mkutano na waandishi wa habari jijini hapa, Kaimu Katibu Mkuu wa Geita Gold, Liberatus Pastory amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika huku akisema kikosi chao kimeshatia nanga jijini Mwanza baada ya mchezo wa Ligi jana ugenini dhidi ya Ruvu Shooting na leo wachezaji wamepewa mapumziko.

Amesema ili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mtanange huo wachezaji wameahidiwa motisha ambayo hakuweka wazi ni ya namna gani lakini akasisitiza itakuwepo na wachezaji wanaitambua kwani wamedhamiria kuisimamisha Yanga na kuvunja rekodi ya kucheza mechi 44 za Ligi bila kufungwa.

"Tumejiandaa kwa mchezo huu, tuna uhakika tutakuwa na mchezo mzuri na kupata matokeo kama ambavyo imekuwa katika Mechi zetu nne zilizopita, tuna imani sisi ndiyo tutasitisha rekodi ya Yanga kutofungwa kwenye ligi wachezaji waendelee kujituma kwa spirit na nguvu ile ili tuweze kutimiza malengo yetu,"

"Kama ilivyokuwa kwenye mchezo na Simba motisha ipo na vijana wanafahamu lakini hatuwezi kuiweka wazi kwamba ni motisha ya namna gani. Kama ilivyokuwa msimu uliopita tulilenga nafasi tano safari hii tunataka nafasi tatu za juu," amesema Pastory ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji ya klabu hiyo.

Kigogo huyo amewaomba mashabiki wa timu hiyo hususan wa mkoani Geita kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono huku akisisitiza kuwa Uwanja wao mpya (Magogo) umefikia asilimia 90, nyasi zimeshapandwa na karibuni wataanza kuzifyema kwa mara ya kwanza na kuondoa magugu ambapo wanatarajia kuanza kuutumia Januari mwakani.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Khalid Bitebo ameipongeza Geita Gold kwa kuuleta mchezo huo jijini hapa huku akiwatoa hofu mashabiki wa soka wanaotarajia kwenda kuushuhudia mchezo huo kuwa ulinzi umeimarishwa na watapata burudani ya kutosha bila kubughudhiwa.

"Sisi kama wenyeji tumejiandaa kuhakikisha mchezo unafanyika kama ulivyopangwa kwa kuweka ulinzi mzuri utakaowahakikishia mashabiki usalama, uwanja uko vizuri unaendelea kufanyiwa maboresho ikiwemo kufyeka nyasi mashabiki waje kwa wingi kuushuhudia mchezo huu," amesema Bitebo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live