Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita haitaki kurudia makosa

Geita Gold Tambo Kikosi cha Geita Gold

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wachimba Dhahabu wa Geita Gold imesema haitaki kurudia makosa tena nyumbani kwa kutamba imejiandaa kukomba pointi tatu itakapovaana na Mbeya City leo mjini Geita.

Geita ilikumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tanzania Prisons mechi iliyopigwa Aprili 24, ikiwa ni ya kwanza kupoteza Nyankumbu tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita na benchi la ufundio la timu hiyo limesema hawataki yawakute tena watakapoikabili City.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote kwani wenyeji Geita wakihitaji kushinda na kujitengenezea mazingira mazuri ya kusalia kwenye nafasi tano za juu, huku City ikitaka kujitoa katika janga la kuangukia kwenye mechi za play-off za kuepuka kushuka daraja.

Geita katika michezo 27 ilizocheza hadi sasa imekusanya pointi 37 ikishinda tisa, sare 10 na kupoteza minane, huku ikifunga mabao 33 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 37, ikiwa nafasi ya tano ya msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na Yanga inayoshuka uwanjani pia leo kucheza na Dodoma Jiji.

Kwa upande wa City ambayo kama ligi ingemalizika leo ingelazimika kucheza play-off ya kubaki kwenye Ligi kwani inashika nafasi ya 13 kwa pointi 27, ikishinda mechi sita, sare tisa na kupoteza 12, ikifunga mabao 30 na kufungwa 40.

Kocha Msaidizi wa Geita, Mathias Wandiba alisema wanatambua mchezo wa leo licha ya kwamba watakuwa nyumbani, lakini utakuwa mgumu kutokana na aina ya timu ambayo watakuwa nayo hivyo wamejipanga kuwakabili.

Alisema hadi sasa maandalizi yao yanaendelea vizuri wamejiandaa vyema kutumia uwanja wao wa Nyankumbu na kubakisha alama tatu nyumbani ili kuweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kusalia katika nafasi ya tano ambayo wapo sasa.

"Tuko vizuri vijana wako katika morali ya juu kuhakikisha tunashinda na kuwafurahisha mashabiki lakini pia kuendelea kuwa juu kwenye msimamo "alisema Wandiba.

Kwa upande wa nyota wa timu hiyo, Geofrey Manyasi alisema kama wachezaji wamejiandaa vyema kupambana na kushinda dhidi ya timu ngumu ya City, pia michezo yote mitatu iliyosalia kwao.

Alisema japo mchezo huo utakuwa mgumu lakini kama wachezaji kwa namna ambavyo wamejipanga anaamini ushindi utakuwepo na kila shabiki atakayejitokeza kwenye uwanja wa Nyankumbu ataondoka na furaha.

Chanzo: Mwanaspoti