Geita Gold imekubali kipigo cha pili mfululizo katika Uwanja wa Nyankumbu kwa kuchapwa bao 1-0 na Mbeya City na kufanya dimba hilo lililokuwa gumu kwa wapinzani wake kutotisha tena.
Matajiri hao wa Dhahabu wamepoteza leo Mei 12, 2023 katika mchezo wa raundi ya 28 ya Ligi Kuu Bara ambao umechezwa uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuanzia saa 8 mchana.
Bao pekee kwenye mchezo wa leo limefungwa na George Sangija dakika ya 56 akimalizia pasi safi ya kisigino kutoka kwa Sixtus Sabilo.
Assisti hiyo ya Sabilo ni ya saba msimu huu kwenye Ligi huku akiwa amefunga mabao tisa ambapo anakuwa amehusika moja kwa moja kwenye mabao 16.
Kipigo ilichopata Geita Gold, ni cha pili mfululizo nyumbani Nyankumbu baada ya mchezo uliopita kuchapwa mabao 3-1 na Tanzania Prisons, ikiwa ni mara ya kwanza katika misimu mitatu na nusu kwa timu hiyo kuruhusu vipigo katika uwanja wa nyumbani.
Ushindi huo unafufua matumaini ya Mbeya City kutoshuka daraja msimu huu, ambapo imepanda hadi nafasi ya 12 ikifikisha pointi 30 kutoka nafasi ya 14 ilipokuwa kabla ya mchezo wa leo na pointi zao 27.
Pia, ni ushindi wa pili kwa Mbeya City kati ya michezo sita iliyozikutanisha timu hizo, ambapo Geita Gold imeshinda mara moja na sare tatu huku yakifungwa mabao saba kukiwa hakuna kadi nyekundu.
Licha ya kichapo hicho, Geita Gold inaendelea kukamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 37, ikishinda mechi tisa, sare 10 na kupoteza tisa huku ikibakiwa na michezo miwili ambayo itachezwa ugenini dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar.
Bao ililofungwa leo, Geita Gold ni la 38 msimu huu kwenye ligi katika mechi 28 ilizocheza ikiwa ni timu ya nne iliyoruhusu mabao mengi nyuma ya Mtibwa Sugar (41), Mbeya City (40), Polisi Tanzania (39) na Ruvu Shooting (39), huku ikifunga mabao 33.