Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita Gold yapata ushindi baada ya siku 100, yazishusha timu nne

Geita Gold Fccccc Geita Gold yapata ushindi baada ya siku 100, yazishusha timu nne

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya ukame wa takribani siku 100 sawa na miezi mitatu, Geita Gold imevuna ushindi wake wa pili kwenye Ligi Kuu Bara, ikifufua matumaini ya kufanya vizuri na kuondoa presha kwa wachezaji na benchi la ufundi lililopo chini ya Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Geita Gold imepata ushindi huo leo Novemba 22, 2023 baada ya kuinyuka JKT Tanzania kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Nyankumbu, mkoani Geita, mchezo huo wa mzunguko wa 10 umechezwa kuanzia saa 10 jioni.

Mara ya mwisho Geita Gold kushinda mechi ya Ligi Kuu Bara ilikuwa Agosti 15, mwaka huu ilipoichapa Ihefu bao 1-0 katika Uwanja wa Highland Estate, Mbeya kwenye mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi wa msimu huu

Ushindi huo wa leo umeipaisha Geita Gold kwa nafasi tano katika msimamo wa ligi ikitoka nafasi ya 15 hadi ya 10 baada ya kufikisha pointi 10 na kuzishusha timu za Namungo, Mashujaa, Ihefu, Coastal Union na Tanzania Prisons.

Katika mchezo huo ambao umekuwa mgumu na kukosa ladha ya kabumbu safi kutokana na uwanja kutoruhusu boli kutembea baada ya mvua kubwa kunyesha, bao pekee la Geita Gold limefungwa na Edmund John katika dakika ya 41 kwa shuti la mbali ambalo limemshinda kipa wa JKT Tanzania, Ismail Salehe na kujaa wavuni.

Bao hilo ni la kwanza kwa Edmund John msimu huu katika mechi tatu alizoichezea timu hiyo baada ya kuzongwa na majeraha ya mara kwa mara akikosa mchezo dhidi ya Yanga, KMC, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa Geita Gold katika Uwanja wake wa nyumbani Nyankumbu msimu huu, ambapo imeambulia sare mbili na kupoteza moja. Katika mechi zake 10, Geita Gold imeshinda mbili, sare nne na kupoteza nne. Kichapo cha leo ambacho imepata JKT Tanzania ni cha nne msimu huu baada ya kufungwa na Yanga mabao 5-0, Dodoma Jiji 1-0 na KMC 2-1. Ambapo imeshinda mechi nne, sare mbili na kupoteza nne.

VIKOSI VILIVYOANZA

Geita Gold: Costantine Malimi, Steven Mgatu, Antony Mlingo, Godfrey Raphael, Kelvin Yondani, Samel Onditi, Seleman Ibrahim, Raymond Masota, Valentino Mashaka, Godfrey Julius na Edmund John

JKT Tanzania: Ismail Salehe, George Wawa, David Brayson, Wema Sadock, Edson Katanga, Hassan Maulid, Ismail Aziz, Said Khamis, Sixtus Sabilo, Najim Magulu na Martin Kigi

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: