Siku chache baada ya kuripotiwa kuwa, nyota wa zamani wa Yanga na Ihefu, Yacouba Songne yupo mbioni kurejea nchini, fasta Geita Gold wamejiongeza kwa kumuita mezani mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso anayecheza soka la kulipwa Djibouti ili kumsajili kupitia dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa wiki ijayo.
Taarifa zilizothibitishwa na pande zote mbili zinasema, Geita inayosaka washambuliaji wawili wa kukiongezea nguvu kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Bara na wameshaanza mazungumzo hayo na nyota huyo wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana.
Yacouba anayeitumikia Arta Solar7 ya Djibouti anataka kuondoka nchini humo baada ya kuona soka la nchi hiyo ni laini likikosa ushindani mkubwa kama ambavyo alitegemea huku akiwa kwenye kiwango kizuri tu tangu atue nchini humo ameshafunga mabao manane.
Geita imemvamia Yacouba haraka na mabosi wa klabu hiyo wakianza naye mazungumzo kwa siri ili waboreshe safu yao ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikikosa makali kwenye mechi zao za ligi msimu huu.
"Tulishaongea na kocha na alimpitisha unajua huyu ni mchezaji ambaye ligi ya hapa anaijua vyema na ameonyesha kiwango sahihi ngoja tuone tutafikia wapi naye," amefichua mmoja wa mabosi wa juu wa klabu hiyo, huku Yacouba, ameithibitisha kuwa, ni kweli anazungumza na klabu hiyo, japo bado hawajafikia mwisho.
"Ni kweli Geita, imenitafuta kuna kiongozi wao tunaendelea kuzungumza, ila sijajua muafaka utakuwaje, naendelea kucheza hapa nikisubiri mazungumzo hayo yakikamilika," amesema Yacouba aliyeifungia Yanga mabao manane katika msimu wa mwaka 2020-2021 kabla ya kuumia na kukaa nje kwa mwaka na nusu kisha kuhamia Ihefu aliyeifungia mabao matatu.